Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imemwachia huru raia wa Nigeria, Ejiofor Henry Ohagwu baada ya kusota kwa takribani miaka 10 katika Magereza ya Tanzania akitumikia kifungo cha maisha jela kwa kupatikana na dawa za kulevya.
Januari 2, 2016, Ohagwu alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, akituhumiwa kusafirisha gramu 4,197.42 za dawa za kulevya aina ya heroin hydrochloride kwenda Nigeria kupitia JNIA.
Sababu kuu tatu zilizomweka huru ni kutoorodheshwa kwa vielelezo viwili wakati wa mwenendo wa ukabidhi (committal proceedings) na kukatika kwa mnyororo wa utunzaji wa kielelezo (chain of custody) ambacho ni dawa hizo.
Ushahidi uliotolewa na mashahidi wa Jamhuri ulidai kuwa siku ya tukio, raia huyo wa Nigeria alikuwepo eneo la ukaguzi wa mizigo kwa kutumia mashine (baggage scanner section) katika eneo la wasafiri wa kimataifa, akisafiri kuelekea Nigeria.
Wakati mizigo yake ikikaguliwa, ilidaiwa vitu vilivyotiliwa shaka vilionekana katika mabegi yake mawili na katika ukaguzi uliofanywa, kulipatikana pakti tatu zilizokuwa na unga unga katika kila begi na kwamba, Ohagwi alijaribu kutoroka.
Hata hivyo, shahidi wa tano na wa saba wa Jamhuri walifanikiwa kumkamata na katika upekuzi, alikutwa na hati ya kusafiria, simu za kiganjani, Dola 475 za Marekani, pesa za Nigeria (Nigerian Naira) 2,050 na pesa ya Tanzania Sh7,000.
Shahidi wa nne alifunga upya unga uliokamatwa na kuuweka katika bahasha na kumkabidhi shahidi wa tatu kwa ajili ya kuutunza na baadaye ulipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kupokewa kisha ufanyiwa uchunguzi wa kimaabara.
Uchunguzi huo ulithibitisha kuwa, unga ule ulikuwa ni dawa za kulevya aina ya heroin na baadaye dawa hizo zilitolewa kortini kama kielelezo namba P1 kisha maelezo ya mshitakiwa yanayodaiwa alikiri, yalipokewa kama kielelezo P6.
Pamoja na mshitakiwa kuyakataa maelezo hayo na kuyakana mabegi yale kuwa hayakuwa yake, Jaji Obadia Bwegoge wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, alimtia hatiani kwa kusafirisha dawa za kulevya na kumfunga kifungo cha maisha.
Hoja na ubishani kisheria
Hakuridhika na hukumu hiyo na kuamua kukata rufaa Mahakama ya rufani akijiwakilisha mwenyewe kortini huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na mawakili waandamizi wa Serikali, Daisy Makala na Edith Mauya.
Katika sababu zake za rufaa, aliegemea hoja sita, moja ni kwamba dawa za kulevya aina ya heroin zilizokuwa kielelezo P1, hakikuwa kimeorodheshwa katika mwenendo wa ‘committal’ katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Sababu ya pili ni kuwa, utaratibu wa kutoa kielelezo P1 na P2 mahakamani ulikiukwa, tatu ni kuwa mnyororo wa utunzaji wa ulikatika na sababu ya nne ni kwamba, yeye hakuwa mmiliki wa mabegi mawili yanayodaiwa kuwa na dawa.
Mbali na sababu hizo, sababu ya tano aliyoiegemea ni kuwa ushahidi uliomtia hatiani ulikuwa hauaminiki na ulijaa kujikanganya na sita ni kwamba, ushahidi wa upande wa utetezi haukuzingatiwa wakati wa kutoa hukumu hiyo.
Wakijibu hoja hizo, mawakili wa Jamhuri walisema kielelezo P1 hakikuorodheshwa wakati wa committal lakini kilioneshwa kuwa ni ushahidi halisi, lakini pia kilitajwa pamoja na vielelezo vingine katika ushahidi wa nyaraka katika shauri hilo.
Kuhusu utoaji wa kielelezo P1 na P2, mawakili hao walisema ilikuwa ni sahihi kwa shahidi wa kwanza kuvifungua kabla ya kuvitoa kama kielelezo huku wakikiri kuwa, mnyororo wa kielelezo kutoka kwa shahidi wa tatu kwenda wa kwanza ulikatika.
Kulingana na rekodi, baada ya shahidi wa kwanza kumaliza uchunguzi wa kimaabara, alikirudisha kielelezo P1 wa shahidi wa tatu ambaye ni mtunza vielelezo, lakini hazioneshi kilirudije tena kwa shahidi huyo akakitoa kortini.
Hata hivyo, walisema kukatika kwa mnyororo huo hakukuathiri ukweli wa ushahidi kuwa ni mrufani alikamatwa uwanja wa ndege akiwa na dawa hizo.
Kuhusu nani alikuwa mmiliki wa mabegi hayo mawili, mawakili hao walikiri kuwa mabegi hayo hayafanyi sehemu ya ushahidi kwa kuwa hayakutolewa kama kielelezo na kwamba hata bila hayo mabegi, ushahidi unaonesha ni ya kwake.
Wakijibu hoja ya mkanganyiko wa ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri, mawakili hao walisema hawajaona mkanganyiko huo na pia wakisisitiza kuwa, utetezi wa mshitakiwa katika kesi hiyo ulipimwa na kuonekana hauna maana yoyote.
Katika hukumu yao ya Oktoba 17, jopo la majaji watatu wa Mahakama ya rufani, Dk Marry Levira, Leila Mgonya na Gerson Mdemu, walisema kwa kupitia kumbukumbu za rufaa, hakuna ubishi kuwa mrufani alikamatwa JNIA.
Hata hivyo, walisema hoja inayohitaji kujibiwa ni kama kweli mrufani alikamatwa akisafirisha dawa hizo katika uwanja huo na katika kujibu hoja hiyo, watajiegemeza katika kupitia hoja za rufaa zilizowasilishwa kwao na raia huyo wa Nigeria.
Wakirejea kumbukumbu inayohusiana na mwenendo wa ukabidhi Juni 12, 2017, hakuna vidhibiti halisi (physical evidence) vilivyoorodheshwa ili kumfanya mrufani aelewe kuwa kielelezo P1 kilikuwamo katika ripoti ya mkemia mkuu.
Majaji hao walisema mwenendo huo unasomeka tu kuwa kutakuwa na vielelezo halisi ambavyo vitawasilishwa wakati wa usikilizwaji wa kesi, hivyo wameridhika kuwa kielelezo P1 cha upande wa mashitaka hakikuorodheshwa siku hiyo.
“Kama tulivyoonesha, kielelezo P1 kilipata njia yake katika ushahidi bila kutajwa au kuorodheshwa wakati wa ukabidhi (committal) wa mrufani. Hata mabegi ambayo dawa hizo zilidaiwa kupatikana, hayakutolewa kama ushahidi.
“Sababu ya kuyakataa mabegi hayo kama ushahidi ni kwamba, hayakuwa yametajwa au kuorodheshwa wakati wa shauri la makabidhiano,” walisisitiza majaji hao katika hukumu yao iliyowekwa mtandaoni Oktoba 18,2025.
“Wakili wa Serikali anasema hata bila hayo mabegi ushahidi unaonesha ni mabegi yake. Tumeshindwa kukubaliana naye kwa sababu mabegi hayo yalikuwa au yalipaswa kuwa sehemu ya kutengeneza ushahidi wa kesi,”walieleza.
Kuhusu kukatika kwa mnyororo wa kielelezo P1, majaji walisema wanakubaliana na wakili wa Serikali kuwa, ulikatika kwani shahidi wa tatu ndiye alikipeleka kwa shahidi wa kwanza, lakini hakuna ushahidi kilirudije kwa shahidi wa kwanza.
Majaji hao walisema sababu hizo zinatosha kubatilisha kutiwa hatiani kwa mshitakiwa na kubadilisha hukumu na adhabu aliyopewa na kuamuru aachiliwe mara moja kutoka gerezani isipokuwa kama anashikiliwa kwa makosa mengine.