Dar es Salaam. Hatimaye mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, umezikwa leo Jumapili Oktoba 19, 2025 nyumbani kwao Kang’oka Jaramongi, Kaunti ya Siaya katika eneo alilozikwa baba yake.
Odinga akiwa na umri wa miaka 80, alifariki dunia nchini India Oktoba 15, 2025 wakati akipatiwa matibabu.
Maelfu ya wananchi wa Kenya pamoja na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya Kenya, wameungana na familia katika viunga vya chuo kumzika waziri mkuu huyo mstaafu wa Kenya.

Akizungumza katika maziko hayo, Rais wa Kenya, William Ruto amesema Taifa la Kenya linabubujikwa na machozi, vilio na huzuni kwa sababu ya kupoteza shujaa mkuu, mtu aliyemtaja kuwa wengi walimuona kama rais wa wananchi.
“Ninaweza kusema kwa ujasiri kwamba Raila hakuwa mhandisi tu; alikuwa mhandisi wa siasa. Miongoni mwa wanafunzi wake ni mimi, William Samoei Ruto. Katika uchaguzi uliopita wa 2022, wale waliokuwa wakiniunga mkono walikuwa na wasiwasi, lakini sikutetereka na ushindani, kwa sababu haikujalisha matokeo yangu kwa sababu Raila angeshinda, au mwanafunzi wake wa kisiasa angeshinda.
“Sikuwa na wasiwasi kwa sababu nilijua kuwa alichopanga kwenye Ilani ya Azimio ilikuwa sawa na nilichopanga kwenye Ilani ya Kenya Kwanza,” amesema Rais Ruto.
Akielezea namna alivyopokea taarifa ya kifo cha Raila, Rais Ruto amesema: “Tulikuwa tunapanga kuhudhuria Maonesho ya Biashara ya Siaya. Hata hivyo, saa 6:40 asubuhi, Oburu alinitumia ujumbe mfupi wa maandishi kwenye WhatsApp na kusema kuwa, kaka yangu alikuwa mahututi.
“Nilidhani tumezungumza na baba, ambaye alikuwa ametuambia kwamba kila kitu kilikuwa sawa. Niliwapigia simu baadhi ya watu, lakini hawakuweza kuniambia hali ya Raila. Dakika kumi baadaye, Oburu alinipigia simu kunijulisha kwamba, inaonekana tumempoteza Baba. Nilimwambia Winnie asiniambie habari mbaya, lakini kwa bahati mbaya, habari hizo mbaya zilikuwa za kweli.”
Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo amesema: “Nilikuwa na Raila Jaramogi Oginga Odinga alipozikwa hapa. Nilikuwa mgeni wa heshima na Raila Odinga ndiye aliyefanikisha hilo.
“Tangu wakati huo, urafiki na udugu wetu umeongezeka, tumefanya kazi pamoja kwa manufaa ya nchi zetu mbili na Afrika nzima. Kwa miaka mingi, nimemfahamu Raila vizuri sana, jambo moja ambalo hukuweza kuliondoa Raila, lilikuwa mapenzi yake makubwa kwa Afrika,” amesema Obasanjo.

Siasa za Afrika zitakavyomkumbuka Odinga atakumbukwa kama kinara wa upinzani na mwanasiasa aliyeshiriki uchaguzi kwa zaidi ya miongo mitatu, amekuwa nembo ya mapambano ya kidemokrasia nchini humo.
Pia, anatajwa kuwa kiongozi aliyejitolea kwa masilahi ya taifa, mara nyingi amehatarisha maisha yake katika harakati za kupigania haki, usawa na utawala bora ikiwamo suala la katiba mpya ya Kenya.
Licha ya kushirikiana na serikali tatu kati ya nne zilizopita nchini humo, Raila aliendelea kuchukuliwa na wengi kama sauti kuu ya upinzani na mlinzi wa demokrasia.
Oburu Ng’ong’a Odinga ndugu wa Odinga ambaye ni seneta wa Kaunti ya Siaya, amesema Rais Ruto ndiye aliyepanga na kulipia safari ya Raila kwenda India.

“Sijui ningefaulu kuandaa haya bila usaidizi wa serikali na Dk Ruto,” amesema Oburu mwenye umri wa miaka 82.
Dada mdogo wa Odinga, Ruth Odinga amesema anawashukuru waliokuwa na Raila hadi mwisho huku akisema, haikuwa kazi rahisi kuwa naye hadi dakika ya mwisho alipofariki dunia.
Winnie Odinga, mtoto wa Raila amewashukuru waliosimama bega kwa bega na baba yao hadi umauti ulivyomfika wakiwamo wafanyakazi wake wa karibu, huku akisema, “mfalme, amekufa lakini taji litaishi kwa muda mrefu. Nimevaa nguo nyeupe kwa sababu tumemuomboleza baba kwa siku tatu zilizopita, lakini leo hatuombolezi; tunasherehekea maisha mazuri. Tunamsherehekea akiwa na miaka 80. Tunamsherehekea baba na urithi wake.”
Mjane wa Odinga, mama Ida Odinga amesema aliolewa na mhandisi ambaye aliendelea na ‘uhandisi wa siasa’ za Kenya.
Amesema mumewe anajua yuko vizuri pale alipo, “ninaomba kwamba, wakati wangu utakapofika, nitaungana naye huko mbinguni. Ulale salama.”