Samia aendelea kusaka kura, abisha hodi Sumbawanga Mjini

Sumbawanga. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan leo Jumapili Oktoba 19, 2025 anaendelea na kampeni zake za kusaka kura na atahutubia mkutano utakaofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Kizwite, Sumbawanga Mjini.

Samia anatarajiwa kufanya mkutano mmoja, baada ya jana kufanya mikutano mitatu mkoani Katavi na Rukwa.

Alianza kampeni zake za jana katika Uwanja wa Azimio, Mpanda Mjini (Katavi), kisha kuendelea Kibaoni, Mpimbwe na kumalizia mji wa Namanyere wilayani Nkasi, mkoani Rukwa.

Tayari maelfu ya wananchi wako katika viwanja vya Kizwite wakisubiri kumsikiliza mgombea huyo wa CCM akiwasilisha sera na Ilani ya Uchaguzi ya chama chake kwa mwaka 2025–2030.

Aidha, viongozi mbalimbali wa chama na Serikali wamewasili katika eneo la mkutano, wakiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk Asha-Rose Migiro, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, pamoja na viongozi wengine wa chama na serikali.

Mmoja wa wananchi waliofika katika viwanja vya Kizwite, Jumanne Abdallah akizungumza na Mwananchi amesema anahudhuria mikutano ya wagombea wa urais wa vyama vyote wanaofika kunadi sera zao.

Abdallah anasema lengo lake ni kutaka kusikia sera na ahadi za wagombea hao, ili Oktoba 29 ikifika, akichague chama na mgombea atakayeridhika naye.

“Niko hapa tangu asubuhi ili kumsikiliza mgombea na Ilani ya chama chake, ili Oktoba 29, 2025 nifanye maamuzi sahihi kwa kuchagua kiongozi atakayeniletea maendeleo,” amesema mwananchi huyo.