Samia atoa matumaini ununuzi wa mahindi

Sumbawanga. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amemtaka Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, kuangalia namna ya kupata fedha ili Serikali iendelee kununua mahindi kwa wakulima.

Kauli hiyo ya Samia inakuja takriban miezi minne tangu Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ilipoacha kununua mahindi kwa wakulima, baada ya kumalizika kwa bajeti iliyopangwa na Serikali kwa mwaka huu wa fedha.

Agizo hilo la Samia limetokana na ombi la mgombea ubunge wa Sumbawanga, Mapinduzi Hilaly, aliyeomba NFRA iendelee kununua mazao, hasa mahindi, kutoka kwa wakulima ili wasiuze kwa hasara kwa walanguzi.

Samia ametoa maelekezo hayo leo, Oktoba 19, 2025, alipozungumza na wananchi wa Sumbawanga mkoani Rukwa, katika mkutano wake wa kampeni.

Ingawa bajeti ilishaisha, amemtaka Dk Mwigulu kuangalia uwezekano wa kupatikana fedha ili Serikali iendelee kununua mahindi kwa wakulima.

“Niwaombe kapekueni muone uwezekano, tuendelee kununua mahindi kwa wakulima,” amesema.

Ameeleza kuwa wananchi wameendelea kuwa na mazao hayo kutokana na ruzuku ya mbolea iliyosababisha uzalishaji kuongezeka.

“Tatizo ni kwamba tumetoa mbolea nyingi, watu wamezalisha lakini bado hatujapiga udongo vyema, tumeleta ugani, watu wamezalisha kwa wingi. Sasa uzalishaji kwa wingi unahitaji mambo mawili maghala ya kutosha kuhifadhi, na fedha za kununua mahindi kutoka kwa wakulima,” amesema.

Hata hivyo, amesema nafasi zaidi ya kuhifadhi mahindi yatakayonunuliwa sasa itapatikana baada ya kuuza yaliyopo nje ya nchi.

Katika hotuba hiyo, Samia amesema mpango wa Serikali ni kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inakuwa karibu na wananchi na kwamba hatanii katika hilo.

Katika gridi hiyo ya taifa ya maji, amesema analenga vyanzo vikuu vya maji viwe Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria, ili kuwa na hifadhi kubwa ya maji.

“Tunapozungumza kuhusu maji safi na salama, hatutanii. Tumejipanga kutumia fedha nyingi kufanikisha gridi ya Taifa ya maji, ili kila Mtanzania awe karibu na huduma hiyo,” amesema.

Kwa upande wa sekta ya umeme, amesema tayari nusu ya vitongoji nchini vimeshaunganishwa na huduma hiyo, na kufikia mwaka 2027, nchi itakuwa na umeme wa uhakika.

“Kukizimwa lazima kutolewe sababu za kufungwa, labda ni matengenezo au kuna kitu kipya kinawekwa, lakini mwaka 2027 tutakuwa na umeme wa uhakika,” amesema.

Samia amewataka wanaobisha kuhusu mkakati wake wa kuanzisha kongani za viwanda kila wilaya, wakaangalie kilichofanywa na Serikali mkoani Mtwara.

Amesema katika miaka mitano ijayo, Serikali itahakikisha inaanzisha kongani za viwanda ili kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa katika eneo husika.

“Kuna watu wanaweza kusema hizi ni stori tu, haiwezekani. Nataka kuwaambia tumeanza kule Mtwara kwenye korosho. Kuna eneo kubwa ambalo ni kongani ya viwanda vya kubangua korosho. Tulikuwa tunasafirisha korosho na maganda yake, kumbe sasa tunasafirisha kazi, nishati na mambo mengi. Sasa watu watapata yale yote wanayoyapata hapa ndani ya nchi,” amesema.

Pia ameahidi kujenga barabara ya Kibaoni-Majimoto-Muze-Kiliamatundu, akisema ana historia nayo hivyo ataisimamia kwa nguvu.

Sababu ya hilo, amesema ni kile kilichotokea mwaka 2020 wakati wa kampeni za urais, alipozuiwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwenda eneo la Muze kwa barabara.

Amesema hatua hiyo ilisababisha atumie helikopta kwenda Muze, huku wasaidizi wake wakitumia njia ya barabara, na waliporudi kila mmoja alitoa ushuhuda mbaya kuhusu hali ya barabara.

“Kurudi, kila mtu jasho linamkatika. Kwa bahati mbaya, wakati wa kupanda mlima, gari moja likirudi, ilibidi wawahi kuipangia mawe. Kwa hiyo, yaliyotokea wakati ule sitaki yatokee tena. Barabara hii nitaisimamia kwa nguvu kubwa, tuhakikishe watu wanashuka kule Muze wakiwa na uhakika wa safari,” amesema.

Ameahidi kujenga stendi ya mabasi ya Laela katika Halmashauri ya Sumbawanga na Barabara ya Matai-Kasesya yenye urefu wa kilomita 50.

Amesema Serikali yake itaangalia uwezekano wa kujenga kilomita 10 za barabara katika Mji wa Kalambo, huku nyingine zikijengwa kwa changarawe ili zipitike mwaka mzima.

Kuhusu maeneo yanayofungua fursa za kiuchumi, amesema Rukwa ina soko la madini na vituo sita vya ununuzi wa madini, na wawekezaji 10 wameonesha ishara ya kuwekeza kwenye sekta hiyo, huku majadiliano yakiendelea.

Amesema tayari kuna wawekezaji wameonesha kuvutiwa na uwekezaji katika madini ya shaba mkoani humo na watajenga viwanda baada ya mazungumzo kukamilika.

Awali, mgombea ubunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, aliwataka wafanyabiashara wa mahindi nchini kuchangamkia fursa ya biashara ya zao hilo nchini Malawi, ambapo mahitaji ni zaidi ya tani 200,000.

“Wanataka zaidi ya tani 200,000 za mahindi. Msipoenda kuuza, tutairuhusu NFRA wakauze, lakini nawapeni dili wafanyabiashara Tanzania acheni kuwa madalali wa watu kutoka nje,” alisema.