Washington. Ili kuhakikisha inatekeleza azma yake ya kusaidia harakati za maendeleo kwa Tanzania na mtu mmoja mmoja, Benki ya CRDB imesaini ushirikiano wa kimkakati wenye thamani ya Sh300 bilioni.
Ushirikiano huo unaihusisha CRDB na taasisi tatu za kimataifa za fedha na maendeleo, ikiwa ni hatua muhimu katika safari yake ya kuendeleza ujumuishwaji wa fedha na maendeleo endelevu barani Afrika.
Hati za makubaliano hayo zilisainiwa wakati wa jukwaa la wabia na wawekezaji lililofanyika kando ya mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) jijini Washington, Marekani.
Jukwaa hilo la kimataifa, lililoandaliwa na Benki ya CRDB, liliwakutanisha wawekezaji wa kimataifa na viongozi wakuu wa Serikali kutoka Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Mikataba hiyo imesaini na mashirika ya FinDev ya Canada, DEG (KfW Group) ya Ujerumani na Shelter Afrique Development Bank (ShafDB).
Makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, pamoja na viongozi wakuu wa taasisi washirika: Mkurugenzi Mtendaji wa FinDev Canada, Lori Kerr; Mkurugenzi Mtendaji wa DEG, Roland Siller na Mkurugenzi Mtendaji wa Shelter Afrique Development Bank, Thierno-Habib Hann.
Kupitia makubaliano hayo, Nsekela amesema FinDev ya Canada itajikita kwenye ukuaji jumuishi, ambapo CRDB imepata uwezeshwaji wa Sh150 bilioni zinazolenga kupanua mikopo kwa wajasiriamali wachanga, wadogo na wa kati (MSMEs).
Katika hatua hiyo, msisitizo utakuwa kwenye biashara zinazoendeshwa na wanawake na miradi inayohimili mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wa DEG, makubaliano yake na CRDB yatajikita kwenye uwezeshaji wa biashara ndogo na za kati SME, ambapo kiasi cha Sh125 bilioni kitatumika kwa ajili ya mikopo midogo, lengo likiwa kusaidia ukuaji wa biashara, ubunifu na uzalishaji wa ajira nchini Tanzania.
Kuhusu usawa wa kijamii na makazi nafuu, Nsekela amesema Shelter Afrique Development Bank na CRDB zinalenga kupunguza uhaba wa makazi katika kanda, ambapo kwa kuanzia CRDB imepokea Sh25 bilioni zitakazotumika kwa kampuni tanzu yake nchini DRC.
“Ushirikiano huu unaakisi dira yetu ya pamoja ya Afrika yenye ujumuishi wa kifedha, usalama wa chakula na maendeleo endelevu. CRDB tunaamini huduma za fedha ni chachu ya maendeleo kufungua fursa, kuzalisha ajira na kuleta thamani ya muda mrefu kwa jamii,” amesema.
Amesema kwa sasa Afrika Mashariki inakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya biashara changa, ndogo na za kati, kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, na makazi nafuu.
“Benki ya CRDB imejipambanua kuwa kinara wa mageuzi ya kikanda kwa kuhamasisha upatikanaji wa mitaji, utaalamu na teknolojia ili kuisaidia jamii na wafanyabiashara,” amesema Nsekela.
Kwa upande wake, Thierno-Habib Hann, Mkurugenzi Mtendaji wa Shelter Afrique Development Bank, amesema: “Tunaamini makazi nafuu na miundombinu ya mijini ndiyo msingi wa ukuaji wa uchumi jumuishi na endelevu. Ushirikiano wetu unaakisi dira yetu ya pamoja ya kuelekeza mitaji katika maeneo yenye athari chanya, usawa na ujumuishaji wa kikanda. Kwa pamoja, hatufadhili tu ujenzi wa nyumba, tunafadhili utu, fursa na miundombinu ya Afrika yenye ustahimilivu zaidi.
“Dhamira yetu ya kuhakikisha kila familia ya Kiafrika inapata makazi salama, nafuu na yanayohimili mabadiliko ya tabianchi ni nguzo ya mageuzi endelevu ya mijini.”
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa FinDev, Lori Kerr, amesema ushirikiano huo umejengwa juu ya dhamira ya pamoja ya kuzalisha fursa mahali panapohitajika zaidi.
Amesema kwa kuimarisha ushirikiano huo watakusanya mitaji na kuwekeza katika uwezo wa masoko ya ndani, wajasiriamali na jamii Kusini mwa Jangwa la Sahara.