TMA yatoa tahadhari wakulima, wafugaji Nyanda za Juu Kusini

Mbeya. Wakulima na wafugaji Nyanda za Juu Kusini, wameshauriwa kutumia vyema vipindi vya mvua za wastani, kuhifadhi maji kwenye miundombinu ya mashamba na maeneo ya malisho ili kuepuka migogoro.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), kutoa utabiri wa uchache wa mvua za wastani katika maeneo mbalimbali nchini, zinazo tarajiwa kuanza mapema Novemba 2025 mpaka Aprili 2026.

Meneja wa TMA, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Elius Lipiki ameliambia Mwananchi Digital leo Jumapili Oktoba 19, 2025 wakati akieleza hali ya utabiri na athari zinazoweza kujitokeza.

“Nyanda za Juu Kusini kutakuwa na mvua za wastani na chini ya wastani zitaanza wiki ya pili na tatu ya Novemba 2025, mpaka Aprili 2026 ambazo zitakuwa na athari katika nyanja mbalimbali hususani sekta ya kilimo,” amesema.

Lipiki ametaja miongoni mwa athari ni pamoja na uzalishaji hafifu wa mazao ambao husababisha na ukosefu wa maji yanayo stahimili na kushambuliwa na wadudu waharibifu hususani panya.

Ameshauri mamlaka husuka ikiwepo serikali za mitaa na idara za maafa kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza, sambamba na kuboresha miundombinu ya maji ili kudhibiti magonjwa ya milipuko.

Lipiki, ametumia fursa hiyo kuwataka wakulima na wafugaji kutumia vipindi hivi kuweka mazingira wezeshi ya kutunza rasilimali za maji kwa ajili ya uzalishaji bora, sambamba na kutenga maeneo ya malisho yasiyoingiliana na shughuli za kilimo.

Katika hatua nyingine ameshauri mamlaka za hifadhi kuweka mikakati mapema ya kudhibiti wanyama kutoingia kwenye makazi ya watu kufuata maji na malisho ili kukabiliana na madhara mbalimbali.

“Lakini pia tutoe rai kwa wananchi, taasisi mbalimbali na wavuvi mwambao mwa Ziwa Nyasa, Wilaya ya Kyela kutumia taarifa za TMA ili kubaini mienendo ya hali ya hewa na namna ya kukabiliana nayo,” amesema.

Mkulima wa mazao ya chakula na biashara Wilaya ya Mbeya, Witness Kamwela amesema changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa mwiba mkubwa katika kuzalisha mazao ya chakuka na biashara.

“Serikali ije na suluhisho la uwekezaji kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kuwaondoa kwenye dhana ya kutegemea mvua ambayo imekuwa ya kusuasua miaka kadhaa sasa,” amesema.

Witness, ametoa mfano kwa miaka mitatu iliyopita kwa msimu kama huu mchele plastiki la kilo 20 lilikuwa likiuzwa kati ya Sh30,000 hadi Sh35,000 kulingana na ubora, lakini mwaka huu bei imepaa hadi kufikia Sh42,000 hadi Sh50,000.

Kwa upande wa zao la mahindi limepanda kutoka Sh10,000 hadi Sh17,000 kwa plastiki la kilo ishirini na huenda bei ikapanda zaidi.

Mkazi wa Nonde Jiji la Mbeya, Rehema Mwanjonde amesema mfumo wa bei za bidhaa za vyakula ni changamoto kwa wananchi wa kipato cha chini na kuomba Serikali kutafuta suluhisho kabla ya msimu wa mvua kuanza ili wakulima waweza kuzalisha kwa tija kubwa.