Dar es Salaam. Baada ya kuenea kwa taarifa za kuzuiwa kwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche kuvuka mpaka wa Sirari kuingia nchini Kenya, Idara ya Uhamiaji imesema kiongozi huyo ameondoka nchini kwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani bila kufuata taratibu na Kanuni za Uhamiaji zilizoundwa chini ya Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54.
Taarifa ya msemaji wa Uhamiaji, Paul Mselle imeeleza kuwa Oktoba,18 2025 katika Kituo cha Uhamiaji cha Mpaka wa Sirari mkoani Mara, Heche ameondoka nchini kwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani bila kufuata taratibu na kanuni za uhamiaji.
“Idara ya Uhamiaji inatoa wito kwa raia wa Tanzania na wageni wote wanaotoka na kuingia nchini kufuata taratibu na kanuni zinazoongoza uingiaji, ukaazi na utokaji wa watu nchini, ili kuepuka kutenda kosa na kuchukuliwa hatua za kisheria,” imeeleza taarifa ya Uhamiaji.
Kabla ya taarifa hiyo, Katibu wa Chadema kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami alisema Heche amezuiliwa kusafiri Kwenda nchini Kenya kuhudhuria mazishi ya Raila Odinga.
Alidai Heche amezuiwa mpaka wa Tanzania na Kenya wa Sirari Wilaya ya Tarime akibainisha kwamba Uhamiaji imechukua hati ya kusafiria ya Heche na haijatoa sababu zozote za kwa nini wanamzuia kwenda nchini Kenya.
Habari zaidi juu ya taarifa hiyo endelea kufuatilia Mwananchi.