ZEC yatoa mafunzo kwa Jeshi la Polisi kuelekea uchaguzi mkuu

Unguja. Zikiwa zimesalia siku 10 kufikia Oktoba 29, 2025 ili Watanzania wapige kura,  Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imelitaka Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia usawa bila kuonesha upendeleo.

Imeeleza kuwa, lengo ni kuona jeshi hilo linatenda haki kwa kila mmoja na kuacha alama nzuri baada ya uchaguzi wa mwaka huu.

ZEC imesema iwapo polisi wakitumia weledi bila kutumia nguvu kubwa na kutenda haki bila kupata maelekezo ya watu fulani, hatua hiyo itaondoa malalamiko kwa wadau wa uchaguzi.

Jumatano Oktoba 29, 2025, Watanzania watafanya uchaguzi mkuu wa kuwachagua Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge, wawakilishi na madiwani.

Akizungumza leo Jumapili Oktoba 19, 2025 wakati wa kufungua mafunzo kwa watendaji wa Jeshi la Polisi, mjumbe wa ZEC, Awadh Ali Said amesema ni mwiko kuonesha au kushabikia upande wowote katika mchakato huo.

Amesema kama walivyofanikisha mchakato wa uandikishaji, uchukuaji fomu na sasa kampeni, hali hiyo iwe hivyo hata wakati wa uchaguzi wenyewe.

“Jeshi la Polisi ni mdau mkubwa sana katika uchaguzi, mnawajibu na jukumu la kulinda bila ubaguzi, upendeleo, kukengeuka wala kushabikia upande wowote, badala yake twende kwenye weledi,” amesema kiongozi huyo.

 “Mkikaa katikati bila upendeleo, ushawishi na ubaguzi ndio utaona zoezi (kazi) hili linaaminika hata mtu akishindwa anaridhika kwa sababu ya mazingira mazuri, kwa hiyo Jeshi la Polisi linawajibika usalama unaimarika.

“Kama tulifanikiwa kuanzia uandikishaji mpaka sasa hatukuona malalamiko na vitendo vya upendeleo, basi tutumie busara, hekima na mbinu zilezile ili kumaliza tukio hili salama jambo ambalo litaacha alama kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimefanya kazi yake kwa weledi.”

Said amesema uchaguzi sio tukio jepesi, bali ni mchakato unaogusa hisia, matarajio ya wananchi na mustakabali wa nchi kwa miaka mitano ijayo.

Akitoa mada katika warsha hiyo, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Wilaya ya Kaskazini A, Yalla Makame Haji amesema uchaguzi unawategemea zaidi polisi katika kulinda usalama na amani ya nchi.

“Ni matumaini yetu mtakuwa mmepata weledi wa kutosha katika kusimamia uchaguzi, sasa muende mkafanye kazi kwa kuzingatia maadili na weledi,” amesisitiza.

Mtoa mada mwingine, Mwanamkuu Gharib Mgeni amesema ulinzi na usalama ni muhimu katika mchakato mzima wa uchaguzi.