Busungu wa Ada Tadea aahidi posho kwa wafungwa

Shinyanga. Mgombea urais kupitia Chama cha Ada Tadea, Georges Busungu amesema endapo atachaguliwa kuongoza nchi katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 29, 2025, serikali yake itahakikisha magereza yote nchini yanaboreshwa na kila mfungwa anapata stadi za maisha pamoja na posho ya kila mwezi.

Busungu amesema posho hiyo itatunzwa katika utaratibu maalumu na mfungwa atakapomaliza kifungo chake, atakabidhiwa fedha hizo kama kianzio akitoka gerezani lengo ni kutaka kumuepusha asirudie makosa yaliyomsababisha kufungwa.

Akizungumza leo Jumatatu katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika eneo la Fantom, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, mgombea huyo amesema mpango huo unalenga kupunguza uhalifu wa kujirudia, hasa kwa wafungwa waliokuwa wanatoka magerezani bila kuwa na mtaji au ujuzi wa kujitegemea.

“Serikali yangu itahakikisha magereza yote nchini yanaboreshwa, kila mfungwa atafundishwa stadi za maisha, na kila mwezi atalipwa posho itakayohifadhiwa rasmi. Atakapotoka gerezani, atakabidhiwa fedha zake kama kianzio cha kuanzisha biashara au shughuli halali za kipato. Hatuwezi kuruhusu mtu arudi kuiba kwa sababu hana namna ya kuishi,” amesema Busungu.

Busungu amesema serikali yake pia itaboresha Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha kila kituo cha polisi nchini kinakuwa na vifaa vya kisasa ili kurahisisha utendaji wa kazi.

Amesema kila mkoa utapewa helikopta moja kwa ajili ya kusaidia polisi kukabiliana na matukio ya dharura, uhalifu na uokoaji wa raia katika mazingira hatarishi.

“Tutahakikisha polisi wanakuwa na vifaa vya kisasa. Kila mkoa utakuwa na helikopta ili wanapohitajika kwa dharura, waweze kufika haraka kuokoa watu au kukamata wahalifu. Tunataka Tanzania iwe salama, tusikie habari za maendeleo, si za watu kutekwa au kuumizwa,” ameahidi mgombea urais huyo.

Akiizungumzia sekta ya elimu, Busungu ameahidi serikali ya Ada Tadea itahakikisha elimu inatolewa bure kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu, bila mikopo wala ulazima wa marejesho baada ya wahitimu kuajiriwa.

“Tutaondoa mfumo wa mikopo na badala yake serikali itabeba jukumu la kugharamia elimu. Hii ni haki ya kila Mtanzania, si zawadi,” amesema.

Aidha, amesisitiza kuwa serikali yake itakuwa ya umoja wa kitaifa yenye watendaji kutoka vyama vyote vya siasa, kwa lengo la kuondoa upendeleo, rushwa na ufisadi.

“Serikali ya Ada Tadea itakuwa ya Watanzania wote, si ya chama kimoja. Tutaunganisha nguvu za vyama vyote kwa maendeleo ya nchi,” amesema Busungu.

Kuhusu uchumi, Busungu amesema serikali ya Ada Tadea itahakikisha viwanda vyote vya madini vinamilikiwa na Watanzania, huku wawekezaji wa kigeni wakihusishwa kama wabunifu wa teknolojia pekee.

“Kama ni utaalamu tunao, vijana wetu wamesoma na wana uwezo. Faida ya madini ibaki hapa nyumbani, si kupelekwa Ulaya. Serikali yangu itaondoa mfumo wa sasa unaowaacha Watanzania kuwa watazamaji wa mali zao,” amesema.

Busungu amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura Jumatano Oktoba 29, 2025 na kuichagua Ada Tadea kwa maendeleo ya kweli ya Tanzania.

Katika mkutano huo, mgombea ubunge wa Kahama Mjini kupitia Ada Tadea, Perpetua Reuben amewahimiza wapiga kura kutoendelea kufanya uchaguzi kwa mazoea, akisisitiza umuhimu wa kubadilisha upepo kwa kuchagua wagombea wa Ada Tadea kwa nafasi zote.

“Ndugu zangu, tusipige kura kwa mazoea. Tubadilishe upepo wa kisiasa ili tuone maendeleo ya kweli. Oktoba 29, mjitokeze kwa wingi na kuikabidhi Ada Tadea kura zenu,” amesema.

Kwa upande wake, mgombea udiwani Kata ya Mondo, Zakayo Deogratius amesema endapo ataaminiwa kuongoza kata hiyo, atawaunganisha wananchi wa Mondo na atahakikisha wanaimarika kiuchumi kupitia miradi ya maendeleo itakayobuniwa.