Dk Mwinyi: Zanzibar Sukuk imeongeza imani kwa wawekezaji, kufungua milango mipya

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema kwa mara ya kwanza uwiano wa mapato ya ndani umeongezeka kwa kasi na sasa Zanzibar, inajiendesha kwa sehemu kubwa kwa kutumia rasilimali zake za ndani kutokana na kuweka mifumo imara ya kidijitali na kuziba mianya ya upotevu wa mapato.

Pia, Dk Mwinyi amesema kupitia Zanzibar SUKUK, Serikali imeweza kugharamia miradi mbalimbali ya kimkakati, kuimarisha imani kwa wawekezaji na kufungua milango mipya kwa sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya Taifa.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Oktoba 20, 2025 katika hafla ya kupongezwa kwa mageuzi ya uchumi na fedha, utoaji wa gawio kwa wawekezaji wa Zanzibar SUKUK na uzinduzi wa skimu ya hifadhi ya jamii yenye kufuata misingi ya Kiislam katika viwanja wa Ikulu Zanzibar.

Amesema uchumi wowote imara unahitaji taasisi madhubuti za mapato, hivyo serikali imefanya mageuzi makubwa katika ukusanyaji wa kodi na kuiimarisha Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) na mifumo yake yote ya ndani.

“Tumeweka mifumo ya kidijitali ya ukusanyaji wa kodi ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa mianya ya upotevu wa mapato, imeongeza ufanisi na kurahisisha ulipaji kwa walipakodi,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema hivi sasa Zanzibar inashuhudia matokeo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukua kwa uchumi wa nchi kwa zaidi ya asilimia 7.2 kwa mwaka.

Amesema mageuzi ya uchumi na fedha yaliyoanzishwa nchini yamekuwa ni msingi muhimu wa kuijenga Zanzibar inayoshirikisha wananchi katika ukuaji wa uchumi wa nchi yao

Pia, misingi ya sera madhubuti mifumo ya kisasa na usimamizi makini wa fedha za umma ni miongoni mwa mambo yanayoendelea kukuza uchumi wa Zanzibar.

Amesema jambo jingine ni kuongezeka kwa uwekezaji wa ndani na nje, kudhibitiwa kwa mfumuko wa bei kwa wastani wa tarakimu moja, mapato ya ndani yameongezeka kwa asilimia 278 katika kipindi cha miaka mitano na sekta za huduma utalii, kilimo na uvuvi zimekua kwa kasi.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, mageuzi hayo yamejengwa juu ya misingi ya uwajibikaji, uwazi na matumizi bora ya teknolojia za kisasa.

Akizungumzia kuhusu SUKUK, Dk Mwinyi amesema mwaka 2024 walizindua na mwaka 2025 wanashuhudia tukio lingine muhimu la malipo ya kwanza kwa wawekezaji hao jambo linalothibitisha ufanisi wa serikali katika kusimamia dhamana zake.

Rais Mwinyi amesema kupitia SUKUK, Serikali imeweza kugharamia miradi mbalimbali ya kimkakati, kuimarisha imani kwa wawekezaji na kufungua milango mipya kwa sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya taifa

“Kwa hakika hii ni historia mpya ya kifedha inayotuweka Zanzibar katika ramani ya dunia ya uwekezaji wa sheria za Kiislamu, hivyo kwa mafanikio hayo wana kila haki ya kujipongeza na kuwashukuru wale wote waliofanikisha hayo,” amesema.

Amesema mafanikio ya uchumi shirikishi hayawezi kupatikana bila ya kuwa na mfumo imara wa bima, hivyo kupitia ZIC, Serikali imeanzisha mfumo wa bima ya Kiislamu ambao utakuwa unatoa huduma za bima kwa msingi wa sheria.

Amesema kupitia mfuko huo huduma za afya zimeanza kupatikana kwa urahisi zaidi, vituo vya afya na hospitali vinapata fedha kwa wakati na wananchi wanapata uhakika wa matibabu bora.

Sambamba na hayo, amesema Serikali imefanya mageuzi makubwa katika mfumo wa hifadhi ya jamii nchini ikiwemo kuimarisha utendaji wa mifuko ya hifadhi na kuhakikisha malipo kwa wastaafu yanafanyika kwa wakati, michango inasimamiwa kwa uwazi na faida zinawanufaisha wanachama.

Kwa kutumia mifumo ya kidijitali watahakikisha wafanyakazi wa umma na binafsi wanasajiliwa na kulindwa dhidi ya changamoto za kiuchumi katika uzee, maradhi na majanga.

Akizungumzia uzinduzi wa skimu ya hifadhi ya jamii, yenye kufuata misingi ya sheria, amesema hatua hiyo itatoa fursa kwa Shirika la Mfuko wa hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kuwekeza kwenye maeneo yanayofuata misingi ya sharia na hata masuala ya hija yataweza kufanikiwa kupitia mfuko huo.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya Salum, amempongeza Dk Mwinyi kwa namna alivyoweza kusimamia mageuzi ya kifedha na kiuchumi kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

Amesema: “ni lazima katika nyanja ya uongozi uwe mbunifu na kufikiri ndani ya muda naye ameyafikia hayo kwani wakati anaingia madarakani utaratibu wa kifedha uliokuwepo sio mzuri.”

Mapema, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Aboud Hassan Mwinyi amesema kipindi cha miaka mitano cha Serikali ya awamu ya nane kumefanyika mageuzi makubwa katika sekta za uchumi na fedha ambayo ndio chimbuko la maendeleo nchini.

Amesema kwa kipindi cha miaka mitano mapato halisi yamekua kutoka Sh671 bilioni hadi Sh2.9 trilioni, bajeti ya Serikali kuu ikiongezeka kutoka Sh1.5 trilioni hadi Sh6.9 trilioni huku bajeti ya miradi ikiongezeka kutoka asilimia 24 hadi asilimia 65 na Pato la taifa likiongezeka kutoka Sh4 trilioni hadi Sh6.5 trilioni.