…………………
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Glory Tausi Shayo, ameahidi kufanya mabadiliko makubwa katika sekta za afya, elimu, na miundombinu ikiwa atachaguliwa kuwa Mbunge.
 Akizungumza katika kampeni zake, Tausi amesisitiza kuwa atahakikisha wananchi wengi wanapata fursa ya kuwa na kadi za bima za afya ili kupunguza gharama za matibabu zinazowaumiza wananchi wengi.
Katika kuendelea na ahadi hizo, Tausi pia amejizatiti kuhakikisha kwamba hakuna mtu atakayezuiliwa kupewa maiti yake hospitalini pale ambapo msiba utatokea. “Hatutaruhusu maiti zizuiliwe hospital, tutahakikisha mtu akipatwa na msiban basi anapewa maiti yake,” alieleza.
Aidha, mgombea huyo ameweka bayana ahadi ya kuondoa michango inayotozwa katika elimu bure, kwa lengo la kuhakikisha watoto wa familia maskini wanapata elimu bila vikwazo vyovyote. “Tutahakikisha kuwa elimu bure inatekelezwa kikamilifu,” alisema.
Tausi amezungumzia pia masuala ya ajira, akiahidi kuwa atahakikisha wanawake na vijana wanapata mikopo kutoka halmashauri ili waweze kuanzisha na kukuza biashara, na hivyo kujipatia ajira za kudumu.
Katika upande wa miundombinu, Shayo ameeleza kwamba atafanya juhudi za kutatua changamoto ya upotevu wa maji, akisisitiza kuwa asilimia 42 ya maji inapotea kila mwaka kutokana na miundombinu mibovu. “Tutahakikisha miondombinu ya maji inaboreshwa ili wananchi wasiteseke na ukosefu wa huduma hii muhimu,” alisema Tausi
Kwa kumalizia, Tausi ameahidi kuleta mabadiliko chanya kwa kushirikiana na wananchi ili kuleta maendeleo endelevu katika jimbo la Kawe.
Â