Hesabu za Mgunda akiiwaza tano bora

KOCHA Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda amesema kuanza kwao vibaya msimu huu haina maana wapo kwa ajili ya kugawa pointi kwa wapinzani, bali kuna mabadiliko makubwa na anaona watakuwa bora na timu shindani.

Namungo imekusanya pointi tano kwenye mechi nne za Ligi Kuu Bara msimu huu ikishinda moja, sare mbili na kupoteza moja.

Akizungumza na Mwanaspoti, amesema malengo yao ni kuwa timu shindani na kumaliza nafasi tano za juu kwenye msimamo, licha ya kuanza vibaya.

MGU 02

“Msimu huu umewasha taa nyekundu mapema sana, kila mmoja anaona ukijiandaa vizuri ndiyo utapata matokeo bora, ukiyumba kidogo utaishia kuwa timu ya kugawa pointi kwa wapinzani,” amesema na kuongeza;

“Hatujaanza vizuri, nafikiri ni kwa sababu ya  aina ya timu tulizokutana nazo hadi sasa zilikuwa na mwanzo mzuri, hili limetuamsha na kurudi uwanja wa mazoezi kujisuka vizuri ili kujiweka kwenye nafasi ya ushindani na naamini mwanzo huu ndio darasa zuri kutupa changamoto ya kujipanga.”

“Tuna malengo makubwa, bado ni mapema sana kukubali kushindwa licha ya kupoteza mchezo mmoja na sare mbili, hii haituondoi kuwa kati ya timu shindani,” amesema Mgunda.

MGU 01

Baada ya juzi kutoka sare ya bao 1-1, Namungo inaenda Kigoma kucheza na Mashujaa, mechi ikipangwa kufanyika Oktoba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.

Kabla ya hapo, ilianza kutoka 1-1 dhidi ya Pamba Jiji, ikaichapa Tanzania Prisons bao 1-0, kisha ikafungwa 3-0 na Simba.