Paschal Lutandula(wa kwanza Kushoto) akionja asali baada ya kununua kwa mjasiliamali.
…………………………..
CHATO
KATIKA kile kinachoonekana ni mchaka mchaka wa mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato kusini, Paschal Lutandula, kuyafikia makundi mbalimbali katika jamii ili kuomba uungwaji mkono kwa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amelazimika kuwafikia wauzaji na wanywaji wa pombe za asili.
Mbali na hao, pia amefanya mazungumzo na wanywaji wa pombe za kitaalamu(Kizungu) kisha kuwasisitiza kukipigia kura Chama hicho ifikapo Oktoba 29 mwaka huu.
Lutandula akiwa katika soko kuu la mji wa Bwanga wilayani Chato mkoani Geita, amenunua mahitaji mbalimbali ya kijamii ikiwa ni pamoja na makopa ya mihogo, nyanya, vitunguu na asali kwa lengo la kuwaunga mkono wajasiliamali wadogo katika kukuza mitaji yao.
Kadhalika amelazimika kushiriki matembezi ya takribani km 2 akiwa na mamia ya wanachama na wafuasi wa Chama hicho kuelekea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Karagwe Oil vilivyopo kwenye Kijiji cha Izumangabo mjini hapo.
Mgombea huyo ambaye anaonekana kuungwa sana mkono na wananchi wa Jimbo hilo, amewataka wananchi kutofanya makosa katika kuchagua viongozi kwaajili ya kuharakisha maendeleo ya Jimbo hilo jipya.
Amesema iwapo wananchi wanatamani kuona Jimbo hilo linakimbia haraka kwa maendeleo hawana budi kumchagua mgombea Urais kupitia tiketi ya CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Diwani wa kata ya Bwanga, Sanane Chai pamoja na yeye mwenyewe ili aweze kuwa mwakilishi wao Bungeni.
Amesisitiza kuwa hatokuwa Mbunge wa kusinzia Bungeni badala yake atahakikisha anapigania miradi ya maendeleo ya wananchi hao na kwamba iwapo watampigia kura kuwa Mbunge wao wajiandae kula Bata na kusahau manung’uniko yote ya kukosa huduma muhimu za kibinadamu.
Hata hivyo amewasisitiza kujitokeza kwa wingi siku ya Uchaguzi mkuu ili watimize haki yao ya msingi ya kuwachagua viongozi wanaofaa badala ya kujitumainisha kuwa Chama hicho kimeshashinda kabla ya kuwapigia kura wagombea.
Kwa upande wake Mgombea udiwani wa kata hiyo, amewaahidi wananchi kushirikiana nao kubuni na kuibua miradi itakayo kuwa na manufaa kwa umma.
Vilevile amesema atahakikisha anasimamia vyema fedha za miradi ya umma pamoja na makusanyo ya fedha za ndani za halmashauri ya wilaya ya Chato ikiwa ni pamoja na kudhibiti mianya ya uvujaji mapato hayo unaofanywa na baadhi ya watumishi wa umma wasio waaminifu.
Mwisho.