MRADI WA HEET KUFUNGWA RASMI JUNI 2026 BAADA YA TATHMINI YA AKINA YA UTEKELEZAJI

 

Mratibu wa Mradi wa HEET ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Razack Lokina,akifungua mafunzo ya  siku tano cha Watekelezaji wa Mradi wa HEET,yameandaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia leo Oktoba 20,2025 jijini Arusha.

Na Mwandishi Wetu, Arusha

CHUO  Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeanza mafunzo ya siku tano ya maandalizi ya kufunga Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), yanayofanyika katika Hoteli ya Parrot jijini Arusha kuanzia leo, Jumatatu Oktoba 20, 2025.

Akifungua mafunzo hayo, Mratibu wa Mradi wa HEET ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Razack Lokina,amesema  mafunzo hayo ni muhimu katika kuwajengea uwezo wataalamu wote wanaoshiriki utekelezaji wa mradi huo, ili maandalizi ya kufunga mradi yafanyike kwa ufanisi na kwa kuzingatia miongozo ya Benki ya Dunia.

“Uwekezaji uliofanyika kupitia Mradi wa HEET ni mkubwa, hivyo ni muhimu kuhakikisha mafunzo haya yanatujengea uwezo wa kufanya ufuatiliaji wa karibu wa mambo ya msingi yaliyotekelezwa, pamoja na kuandaa nyenzo za uandishi wa ripoti zitakazowasilishwa kwa Benki ya Dunia. Hatutaki kuwe na kipengele chochote kitakachoachwa bila mpango wa utekelezaji au uendelezaji,” amesisitiza Prof. Lokina.

Kwa upande wake, Mratibu Msaidizi wa Mradi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Evaristo Mtito, ameipongeza UDOM kwa kuandaa mafunzo hayo, akisisitiza  hatua muhimu katika kushughulikia mapema mapungufu ya utekelezaji wa mradi na kuandaa taarifa kamili zinazoonyesha mafanikio, fursa na changamoto zilizojitokeza.

“Ikumbukwe kuwa, endapo kutakuwa na dosari katika usimamizi wa malalamiko, mradi unaweza kuchelewa kufungwa. Hivyo ni vyema kupitia upya kila kipengele kwa mujibu wa mkataba na miongozo ya mfadhili ili kubaini mapungufu na kuyafanyia kazi,” ameeleza Dkt. Mtito.

Naye Mtaalamu wa Masuala ya Jamii kutoka Wizara ya Elimu Bi. Neema Wilson, amesisitiza umuhimu wa kutunza kumbukumbu sahihi za utekelezaji wa mradi, hasa katika maeneo ya ujenzi, pamoja na kuhakikisha vibarua wanalipwa kwa wakati na kwa viwango vilivyokubaliwa, ili kuepusha migogoro au athari za bajeti wakati wa hatua za mwisho za mradi.

Kwa upande wake,  Mtaalamu wa Mazingira Dkt. Julius Elias,amekumbusha umuhimu wa kulinda mazingira wakati na baada ya utekelezaji wa mradi kwa kuhakikisha maeneo ya ujenzi yanaachwa salama bila athari za kimazingira. Amesisitiza kufuata Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake, kusajili majengo OSHA kwa usalama wa wafanyakazi, pamoja na kupata vibali vyote vinavyotakiwa na Benki ya Dunia.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kama sehemu ya maandalizi ya kufunga rasmi Mradi wa HEET, unaotekelezwa katika vyuo vikuu mbalimbali nchini na unatarajiwa kufungwa rasmi mwezi Juni 2026.

Mratibu wa Mradi wa HEET ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Razack Lokina,akifungua mafunzo ya  siku tano cha Watekelezaji wa Mradi wa HEET,yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia leo Oktoba 20,2025 jijini Arusha.

Mratibu Msaidizi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Dkt. Evaristo Mtito, akizungumza wakati wa  Mafunzo ya kufunga Mradi Mradi wa HEET,yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika jijini Arusha.

Mtaalamu wa Masuala ya Jamii kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi. Neema Wilson, akitoa mafunzo kwa washiriki kuhusu masula ya Jamii yanapashwa kuzingatiwa wakati wa kuhitimisha Mradi wa HEET, unaotazamiwa kukamilika rasmi mwezi Juni 2026.

Mtaalamu wa Mazingira kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Julius Elias, akitoa mafunzo kwa washiriki kuhusu mambo msingi ya mazingira ya kuzingatiwa wakati wa kuhitimisha Mradi wa HEET.

Mratibu Msaidizi wa Mradi wa HEET kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Happiness Nnko, akisikiliza kwa makini maelekezo wakati wa mafunzo ya siku tano kuhusu mambo msingi ya kuzingatia wakati wa kufunga Mradi.

Washiriki wa Mafunzo ya kufunga Mradi wakisikiliza mafundisho yaliyokuwa yakitolewa leo katika Hoteli ya Parrot, Arusha.