Mwalimu atua Morogoro akilia viwanda kugeuzwa maghala akitoa ahadi

Morogoro. Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salim Mwalimu amesema tatizo la ukosefu wa ajira katika Mkoa wa Morogoro limetokana na kuuzwa kwa viwanda vilivyokuwa vimeanzishwa mkoani humo miaka ya nyuma.

Mwalimu ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Oktoba 20, 2025, wakati akihutubia mkutano wa kampeni za kunadi sera na ilani ya chama hicho uliofanyika katika viwanja vya Soko la Chief Kingalu, Morogoro.

Amesema wazee wa miaka 60, wanaweza kushuhudia jinsi dunia ilivyokuwa ikiutambua Mkoa wa Morogoro kutokana na wingi wa viwanda na uzalishaji wa chakula, lakini sasa hali imebadilika.

“Ilifika mahali dunia ikaijua Morogoro kwa kuwa na viwanda, lakini leo vimegeuzwa maghala na maeneo ya kufugia baada ya kuuziana. Kisha wanaulizana ajira zinatoka wapi? Tumeua viwanda, biashara na kilimo, halafu tunatarajia neema itoke wapi?” amehoji Mwalimu.

Amesema kutokana na hali hiyo, wananchi wengi sasa hufanya biashara kwa mazoea ili wapate mahitaji ya kila siku kama sukari na mkate kwa watoto, badala ya kuwa na matumaini ya kuwekeza na kuendeleza maisha yao.

“Msicheze na chama kilichopo madarakani ndugu zangu, hakuna nchi inayouza maendeleo wala soko linalouza utajiri. Hakuna mtu atakayetumwa kununua maendeleo nje. Mungu ametupa rasilimali ambazo ndizo zinapaswa kutupeleka kwenye uchumi imara na maendeleo ya kweli,” amesema.

Mwalimu ameongeza kuwa maendeleo na utajiri wa nchi yoyote hutegemea uwezo wake wa kusimamia rasilimali zake na amesisitiza kuwa Chaumma ikiingia madarakani itahakikisha jambo hilo linasimamiwa kwa vitendo.

“Unapoambiwa Marekani au Uingereza ni matajiri, ni kwa sababu wametumia rasilimali zao vizuri. Sisi pia Mungu ametujalia kila aina ya madini, mafuta na gesi. Nenda Arabuni, wanaringia mafuta bila kuwa na ardhi wala watu, lakini sisi tuna vyote hivyo, bado tupo masikini,” amesema.

Akiomba kura kwa wakazi wa Morogoro, Mwalimu amewataka wasimtazame kwa umri wake, bali kwa dhamira yake ya kweli ya kuwaletea maendeleo.

“Watu wa Morogoro, naomba msiniangalie kwa umri. Nipimeni kwa dhamira yangu ya kutaka kubadili maisha yenu. Waliopita walikuwa wakubwa zaidi yangu kwa umri, lakini bado wananchi mnaendelea kutaabika na biashara zimekufa,” amesema mgombea huyo.

Katika hatua nyingine, Mwalimu amedai tangu kuanza kwa kampeni hakuna mgombea ambaye amezunguka nchi nzima kama yeye.

Amesema gari alilopewa na Tume Huru ya Uchaguzi lilikuwa linasoma kilomita 500, lakini sasa limefikia zaidi ya kilomita 10,000, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kufikisha ujumbe wa mabadiliko kwa Watanzania.

“Hatulali usiku, tunazunguka kuelimisha wananchi maana ya kura yake. Maisha yanazidi kuwa magumu, fursa zinapungua. Ni lazima tukubali kubadilika,” amesisitiza Mwalimu.