Tabora. Mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Isenegeja iliyopo kata ya Mwisi, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, William Emmanuel (12), amefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye kisima alipokuwa akichota maji.
Akizungumzia tukio hilo leo Jumatatu Oktoba 20, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema mtoto huyo akiwa na wenzake saba, waliagizwa maji na mwalimu wao katika kisima hicho, ndipo akatumbukia kisimani na kupoteza maisha.
“Hawa watoto walitumwa maji na mwalimu wao na walikuwa kundi la watoto wanane, sasa wakati wanaendelea kuchota maji, mwenzao akatumbukia na kupoteza maisha,” amesema kamanda huyo.
Amesema tukio hilo limesababisha taharuki kwa wazazi na walezi katika kata hiyo, hali ambayo ilisababisha kuitishwa kwa kikao kilichohusisha vyombo vya usalama, wazazi na walezi na uongozi wa shule na hatimaye ikabainika kwamba kifo kilichotokana na ajali tu, hapakuwa na uzembe wowote.
“Niwatoe hofu wananchi kwamba Jeshi la Polisi lipo kazini na hasa kuhakikisha kuwa usalama wa raia na mali zao unakuwepo na kuhakikisha kuwa watu wanaishi kwa amani bila shida yoyote katika maeneo yao,” amesema.
Amewasisitiza wazazi na walezi katika mkoa huo kwamba walimu pia ni walezi wa watoto pindi wanapokuwa shuleni, hivyo wakae nao vizuri kwani ni watu muhimu zaidi kwa malezi ya watoto badala ya kuwachukia pale linapotokea tatizo.
“Walimu huwa ni walezi wazuri tu, kwa hiyo linapotokea tatizo ni vema kulivumilia nakusubiri kulipatia ufumbuzi wake ili kuondoa taharuki kama ambavyo imekuwa katika tukio hili la mtoto Wiliam,” amesema.
Amewashauri walimu katika shule za Mkoa wa Tabora kuambatana na wanafunzi wanapokuwa wanakwenda katika maeneo hatarishi, ikiwemo sehemu zenye mashimo makubwa au visima vilivyo wazi kama kilivyokuwa kisima cha Isenegeja kuachwa wazi.
“Visima vinapaswa kujengewa kuta lakini juu kuwekwa mifuniko ili kuwa salama zaidi kuliko kuachwa wazi au kutokujengewa vizuri,” ameongeza Kamanda Abwao.