RC Songwe aonya watakaovuruga uchaguzi Oktoba 29, 2025

Songwe. Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabir Makame ametoa onyo kali kwa watu wanaodaiwa kupanga njama za kuvuruga uchaguzi unaotarajiwa kufanyika katika siku chache zijazo, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya watakaobainika kuhatarisha amani na utulivu wa mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari  mjini Tunduma mkoani humo leo Jumatatu Oktoba 20, 2025 Makame amesema uchaguzi ni nguzo muhimu ya kidemokrasia inayowapa wananchi mamlaka ya kuchagua viongozi wanaowataka kuwawakilisha kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Makame amesema Serikali imejipanga na kudhamiria kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, amani na utulivu kwa kufuata misingi na kanuni zilizoandaliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Makame amesema kuwa vyombo vya dola vimejipanga kikamilifu kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na haki ikiwa ni Pamoja na kuwadhibiti walio na nia ovu ya kuhatarisha amani iliyopo hapa nchini.

“Kama kuna watu wamejipanga kufanya vurugu siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 msijaribu kwani vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kuwashughulikia na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria,” amesema Makame.

Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kufuatilia kubaini makundi ya watu wanaojaribu kupanga njama za kuvuruga uchaguzi na kwamba yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Baadhi ya wananchi wa Tunduma wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Songwe Jabir Omary Makame katika eneo la kisimani mjini Tunduma.picha na Denis Sinkonde

Makame amesema uchaguzi ni nguzo muhimu ya kidemokrasia inayowapa wananchi mamlaka ya kuchagua viongozi wanaowataka kuwawakilisha kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, hivyo amewasihi wananchi wa mkoa wa Songwe kutumia haki yao ya kikatiba na kidemokrasia kujitokeza kwa wingi kupiga kura kuwachagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano.

“Viongozi wanaochaguliwa ndio wanaobeba dhamana ya maamuzi yanayogusa maisha ya kila Mtanzania na mafanikio ya kila kundi la kijamii, kuanzia wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wachimbaji wadogo wa madini, madereva wa bodaboda, mama lishe, vijana na wanafunzi, yanahusiana moja kwa moja na maamuzi ya viongozi wanaochaguliwa,” amesema Makame.

Makame amesema kuwa tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961, nchi imeendelea kuheshimu misingi ya katiba na demokrasia kwa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano bila kukosa, jambo linalothibitisha ustahimilivu wa mfumo wa kisiasa na umoja wa kitaifa.

Kuhusu mwenendo wa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2025, amebainisha kuwa Mkoa wa Songwe umeendelea kushiriki kikamilifu katika hatua mbalimbali zinazosimamiwa na INEC na wananchi wameonyesha mwamko mkubwa na ushirikiano katika hatua za maandalizi, jambo linaloashiria uchaguzi wa amani na utulivu.

Aidha Makame amewashukuru wadau wote wa uchaguzi wakiwemo vyama vya siasa na wagombea wao, viongozi wa dini, viongozi wa mila, wazee wa kimila, asasi za kiraia, vijana na wanawake kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kuhamasisha amani na ushiriki wa kidemokrasia kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29,2025 ukawe wa amani na utulivu.

Kwa upande wake kiongozi wa mila kutoka kabila la Wanyamwanga, Malinga Mkoma amewataka vijana kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025 akisisitiza kuwa ni jukumu lao kuhakikisha amani inalindwa ipasavyo kwenye maeneo yao.

“Vijana msikubali kuwa mawakala wa kuvunja amani bali tuwe walinzi wa amani ikiwa ni pamoja na kutokukubali kutumika na taasisi ambazo hazilitakii mema Taifa,” amesema Chifu Mkoma.