Samia aahidi kumaliza adha ya mafuriko Bonde la Rufiji

Pwani. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi akipewa ridhaa ya kuongoza kwa kipindi kijacho, Serikali yake itadhibiti adha ya mafuriko katika Bonde la Mto Rufiji, ikiwemo kujenga zuio la mafuriko.

Amesema pia Serikali itatekeleza mradi wa skimu za umwagiliaji maji hekta 13,000 wilayani humo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji maji na udhibiti wa mafuriko.

Samia ametoa ahadi hizo na nyingine zilizoainishwa kwenye ilani ya CCM ya mwaka 2025/30 leo, Jumatatu Oktoba 20, 2025, alipozungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Ujamaa, Ikwiriri katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Samia, ambaye pia ni Rais, amesema akipewa ridhaa, miongoni mwa masuala atakayoshughulikia mbali na uwezeshaji wananchi kiuchumi na huduma za kijamii, atasimamia kikamilifu sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo, ufugaji na uvuvi.

“Kuna mradi tunaokuja nao mkitupa ridhaa, kwa upande wa kilimo, mradi wa umwagiliaji maji na udhibiti wa mafuriko kwenye Bonde la Mto Rufiji. Katika bonde lile, tunakwenda kujenga mabwawa mawili makubwa.

“Pia, tunakwenda kutengeneza skimu za umwagiliaji hekta 13,000, ambazo zinatokana na hekta 60,000 zilizopo kule za kumwagilia,” ameongeza.

Kuhusu ujenzi wa zuio la mafuriko, amesema mkandarasi ameshapatikana na gharama yake ni Sh245 bilioni ambapo pamoja na mradi huo, kilomita 90 za barabara na makalavati zitatengenezwa.

Mgonbea urais kwa tiketi ya CCM,Samia Suluhu Hassan akizungumza katika mkutano wa kampeni leo Jumatatu Oktoba 20,2025 katika uwanja wa Ujamaa,Ikwiriri wilayani Rufiji mkoa wa Pwani,ikiwa ni mwendelezo wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 20,2025

“Ujenzi wa zuio la mafuriko, ile mambo ya mvua roho juu mnaanza kukimbia wajukuu zangu sasa hayapo,” ameongeza.

Samia amesema Wilaya ya Rufiji ni wakulima wazuri wa mazao ya chakula na biashara, ikiwemo korosho, ufuta na mbaazi, na kuwa wilaya hiyo imeongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani 87,829 hadi kufikia tani 112,118, huku korosho ikikua kutoka kilo milioni 2.57 hadi kufikia kilo milioni 4.2 msimu uliopita.

“Korosho zetu zimeanza kuchukua hadhi, zinazalishwa vizuri, lakini ili tuzalishe kwa wingi lazima tulete pembejeo. Tumeamua kutumia fedha nyingi mzalishe kwa wingi, mpige mnada fedha iingie kwa mkulima. Msimu ujao wa korosho, tunatarajia ongezeko zaidi. Mnada wa korosho unakwenda kuanza Oktoba 30, 2025. Tukimaliza kupiga kura Oktoba 29, tupeleke korosho kwenye maghala ili zipigwe mnada,” ameongeza.

Kwa upande wa viwanda, mgombea huyo amewaeleza wananchi kuwa kuna wawekezaji wamepatikana na kuwaomba wawape ushirikiano, kwani hiyo itawapa ajira.

“Tunaleta wawekezaji ili kuinua uchumi wa eneo hili kwa ujumla. Kwenye uvuvi, tulileta boti mbili kubwa za doria, zilizochangia kupungua kwa uvuvi haramu kutoka asilimia 70 hadi 30. Tumeshuhudia kuongezeka kwa mazao ya samaki na uzalishaji wa samaki maji chumvi, toka tani 610,000 hadi tani 900,000,” amesema.

Mgombea huyo wa urais ameahidi katika miaka mitano ijayo kujenga kiwanda cha kusindikiza samaki Kata ya Ikwiriri, na CCM inaahidi kujenga vizimba vitano vya ufugaji wa samaki kwenye kata mbalimbali, ikiwemo Ikwiriri.

Samia amesema Serikali ya awamu ya sita mtazamo wake ni kuleta maendeleo kuanzia vijijini kwa kufanya kazi kwenye ngazi tatu huduma za jamii, uwezeshaji wananchi kiuchumi na sekta zinazokuza uchumi mkubwa wa taifa kuanzia vijijini.

Akizungumza katika mkutano uliofanyika Kibiti, Samia amesema wilaya hiyo ilizalisha ufuta kutoka kilo milioni 5.3 hadi kilo milioni 11.1, na kuahidi katika miaka mitano ijayo wataendelea na ruzuku ya pembejeo na mbolea.

Ameahidi kuboresha barabara za ndani ikiwemo kilomita 42 za maeneo korofi ili zipitike wakati wote, na kuwawezesha wakulima kusafirisha mazao yao, wagonjwa kufika hospitali na wanafunzi kufika shuleni mapema.

Kuhusu maji, amesema walikamilisha miradi 23 na hivyo kuongeza hali ya upatikanaji wa maji kutoka asilimia 47 hadi 74, na kuwa kuna miradi miwili inayoendelea itakayofikisha upatikanaji wa maji kufika asilimia 85, na miaka mitano ijayo watamaliza adha hiyo ya maji.

“Hawa na mimi tutaenda kufanya kazi za Taifa, watasaidia kazi ya Taifa. Najua kampeni hizi vyama vingi tunafanya kampeni, inawezekana vyama vingine, tamaa ya kupata urais hawana, lakini nitoke japo na kata wapate diwani. Sasa mkichanganya mkawatilia rangi nyingine siyo kijani, maendeleo yatachelewa, watakaa kubishana badala ya kujadili maendeleo na kutekeleza. Niwaombe mchague wagombea wa CCM,” amesema.

Mgombea ubunge Jimbo la Rufiji, ambaye pia ni Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa

Awali, mgombea ubunge Jimbo la Rufiji, ambaye pia ni Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, amesema Samia ni mwanamapinduzi wa kiuchumi. Katika kipindi cha miaka minne, wizara hiyo ilitumia zaidi ya Sh6 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali, ikiwemo sekta ya afya, elimu na miradi mingine.

Kuhusu Rufiji, amesema kwa miaka mingi vijana wengi hawakupata elimu, na kuwa akiwa mbunge alikuta shule nne za sekondari, lakini katika miaka minne ya Samia, shule mpya 22 za sekondari zimejengwa wilaya humo, huku shule za msingi zikiwa 63 zikijengwa kutoka 19 zilizokuwapo.

Mgombea huyo amemwomba Samia kuridhia ombi la kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Rufiji ili kuwapunguzia wananchi adha ya kufuata huduma mbalimbali kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kibaha, umbali wa kilomita 400, ambapo wengine wanalazimika kupita Dar es Salaam na wengine Morogoro.

“Kuhusu uchaguzi mkuu, kila mkoa umejipanga vizuri kuhakikisha wanaweka ulinzi kwa Watanzania kwenda kupiga kura Oktoba 29. Niwatoe hofu Watanzania tujitokeze kwa wingi kwenda kumchagua Samia, wabunge na madiwani wa CCM,” amesema.