Dar es Salaam. “Tumempoteza mtoto,” ni kauli ipenyayo kwa uchungu masikioni mwa wazazi, ambao kwa miezi tisa walisubiri kukishika mikononi kichanga chao.
Katikati ya uchungu huo, imeibuka teknolojia mpya ya kitita cha uzazi salama, inayowapa wakunga ujuzi na ujasiri wa kuokoa maisha ya mtoto mchanga aliyepotea awali baada ya kuzaliwa, ndani ya saa 24 au katika siku saba za mwanzo.
Ndani yake kuna kifaa kiitwacho Neo Beat, kilicho kwa mfano wa saa yenye mikanda. Huwekwa kifuani mwa mtoto mchanga baada ya kuzaliwa ili kupima mapigo ya moyo na husoma iwapo kuna uhai kwa mtoto aliyezaliwa akiwa kimya.
Kifaa kikiusoma uhai, mtoa huduma atatumia kifaa hicho sambamba na kifaa maalumu kitakachowekwa mdomoni mwa mtoto au mfuko wa kumpatia hewa, na kuanza ku-pump mapigo ya mtoto yatapanda taratibu kwa kadri anavyoendela mpaka pale moyo wa mtoto utakaposhtuka na atalia, kuashiria kuwa sasa ameanza kupumua.
Ujio wa kifaa hicho cha kiubunifu ni nyenzo muhimu, hasa wakati takwimu zikionesha bado kuna changamoto ya vifo vya watoto wachanga nchini. Katika kila vizazi hai 1,000, hutokea vifo vya watoto 43.
Akizungumza na Mwananchi, Mkunga Muuguzi kutoka Hospitali ya Hydom, Sprina Ryoba, anakielezea kifaa hicho bunifu ambacho kimeletwa na mradi wa Hydom kupitia afua ya Kitita cha Uzazi Salama.

Sprina, ambaye pia ni mwezeshaji wa mafunzo katika mradi wa Kitita cha Uzazi Salama (SBBC), anasema kifaa hicho kimesaidia kuokoa watoto wanaozaliwa wakiwa wameshindwa kupumua ndani ya dakika ya kwanza, ambao awali hawakugundulika kama wangali hai.
“Mwanzo, wauguzi walikuwa wanatumia mkono kushika kitovu na kuona kama mtoto yuko hai. Hospitali ya Hydom wamekuja na kifaa hiki ambacho kimeweza kutusaidia kuwaokoa watoto ambao awali tulikuwa tunashindwa kuwaokoa.
“Hiki kifaa tunakitumia kumwekea tumboni yule mtoto aliyezaliwa amechoka na hapumui. Baada ya kukiweka, kinatuonesha kama mtoto bado yuko hai, na baadaye mtoa huduma atamsadia mtoto kupumua na kuendelea kuishi,” anasema.
Anasema kifaa hicho kimeleta matokeo mazuri,watoto wengi wameokolewa.
“Kwa asilimia 18, tumeokoa vifo vya watoto hawa, na kwa asilimia 40 tumeokoa watoto ambao walipotea ndani ya saa 24. Pia tumeokoa watoto kwa asilimia 16 wale waliopoteza maisha ndani ya siku saba.
“Kwa hiyo unaweza kuona kifaa hiki kimetuokoa sisi watoa huduma kupunguza vifo kwa kujua kwamba mtoto bado yupo hai,” anasema Sprina.
Mkunga Muuguzi kutoka Kahanhara HC, Elina Edson, anasema wameokoa watoto wengi kupitia kifaa hicho.
“Kuna mtoto jana alipata changamoto hii. Nilianza kumpa pumzi, kadri muda ulivyozidi kwenda pumzi ziliongezeka na rangi ikawa inabadilika. Baadaye mtoto akalia kwa fito heart ya 145. Tulifurahi sana, baadaye tukampa mama taarifa kuwa mtoto wako anaendelea vizuri. Alipewa mtoto na kuendelea kumnyonyesha,” amesema Elina.
Mratibu wa kitaifa wa SBBC, Beatrice Wanjiku Githiri, anasema kifaa hicho ni salama na kina ufanisi mkubwa, hivyo kuwaweka watoto na kinamama salama wakati na baada ya kujifungua.
Anasema pia kinaisaidia timu ya watoa huduma za afya kutumia teknolojia hiyo ili waweze kudhibiti matatizo yanayojitokeza mara kwa mara wakati na baada ya kujifungua.
“Tunatoa vifaa hivi vya kibunifu vinavyosaidia kufanya maamuzi bora kwa wakati, ili wawe na maarifa ya kutosha na kuokoa maisha ya mama na watoto zaidi,” anasema.
Beatrice anasema awamu ya kwanza ya mradi huo ilitekelezwa mwaka 2020 hadi Desemba 2023 kwenye vituo 30 vya kutolea huduma za afya katika mikoa mitano ambayo ni Manyara, Mwanza, Geita, Shinyanga na Tabora.
“Awamu ya pili ya kitita inatekelezwa kwenye mikoa ile ile mitano, lakini kwenye vituo 142 vya kutolea huduma za afya. SBBC ni muunganiko wa bunifu mbalimbali; ubunifu wa vifaa vya mafunzo na ubunifu wa ubora endelevu,” anasema na kuongeza kuwa wamefikia kinamama 300,000.
Kitita cha Uzazi Salama (SBBC), kilichohusisha zana za kliniki na mafunzo ya ubunifu kwa ajili ya huduma bora za uzazi na watoto wachanga, kilifanyiwa utafiti kabla.
Mtafiti Mkuu wa programu ya SBBC, Dk Benjamin Kamala, amesema kifurushi hicho kikitumika kwa usahihi, hatari ya kifo cha mama mjamzito au mtoto mchanga wakati wa zamu ya mkunga mwenye vifaa hivyo inapaswa kuwa chini au nadra.
“Wakunga ambao wamefaidika na teknolojia kama hii nchini Tanzania wana ushahidi kupitia utekelezaji wa kitita hiki.”
Pamoja na vifaa vingi vilivyopo sambamba na mafunzo, Dk Kamala amekitaja kifaa cha Neo Beat kwamba husaidia kupima mapigo ya moyo wa mtoto kwa usahihi na urahisi, na hutumika hasa kwa watoto wachanga ambao wanashindwa kupumua wenyewe mara tu baada ya kuzaliwa.