Viongozi wa dini Mwanza watoa tamko la amani kuelekea uchaguzi mkuu

Mwanza. Zikiwa zimesalia siku tisa kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, viongozi wa dini mkoani Mwanza wametoa tamko la kuhamasisha amani na utulivu, wakitoa wito kwa wananchi kujitokeza kupiga kura.

Tamko hilo limesomwa leo Jumatatu Oktoba 20, 2025 na Mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza, Askofu Charles Sekelwa akiwa na viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu mkoani humo wakati wa kongamano la amani.

Katika tamko hilo wamesema wanaungana kwa sauti moja kutoa ahadi na rai kwa Serikali na wananchi wote wa Tanzania kwamba wataendelea kuhamasisha wananchi wa Mkoa wa Mwanza na nchi nzima kujitokeza kupiga kura kwa uhuru na haki Oktoba 29, 2025.

Viongozi hao wa dini wamesema ni wajibu wa kila Mtanzania kutumia haki yake ya kikatiba kupiga kura, wakisisitiza utulivu baada ya upigaji kura.

Baadhi ya viongozi wa dini wakitoa tamko leo Oktoba 20, 2025 kuelekea uchaguzi mkuu wakati wa kongamano la amani lililofanyika mkoani Mwanza.

“Tunawahimiza wananchi wote kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura kumchagua Rais, wabunge na madiwani katika ngazi zote kwa upendo, busara na uwajibikaji.

“Baada ya kumaliza kupiga kura, tunawasihi wote warejee majumbani kwao kwa utulivu, bila vurugu na bila maneno ya chuki ili kudumisha taswira njema ya Taifa letu la amani,” wameeleza viongozi hao katika tamko lao.

Wameongeza kuwa wataendelea kusali na kuomba dua ili uchaguzi ufanyike kwa utulivu wakimuomba Mungu aibariki Tanzania, aendelee kutoa hekima, umoja na amani katika kipindi chote cha uchaguzi na hata baada ya uchaguzi.

“Tukumbuke kwamba amani ni nguzo ya maendeleo, umoja ni nguvu, na upendo ni suluhisho la kila changamoto,” limeeleza tamko hilo.

Awali, Askofu Sekelwa amesema wanapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, Watanzania wana haki ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi wanaowafaa kwa utulivu.

“Tutumie uhuru wetu kwa kutumia fikra sahihi kwa sababu uhuru wa kweli ni mimi kupata nafasi ya kumchagua mtu atakayeniongoza…kupiga kura ni haki ya kikatiba, kumchagua kiongozi unayemtaka ni haki ya kikatiba,” ameeleza.

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo, Sheikh Hassan Kabeke amesema pasipo amani hakuna haki, akisisitiza kabla ya haki ni lazima amani iwepo.

“Haki haiwezi kuwepo pasipo na amani…ni haki yetu kusali kwa sisi Waislamu mara tano, wenzetu Wakristo siku ya Jumapili… tuulizaneni ikiwa pamechafuka nani ataenda kuswali? Amani ndiyo jamvi la haki…wenzetu wa Gaza leo wanatafuta amani au haki? Amani kwanza,” ameeleza.

Mjumbe wa kamati hiyo, Mchungaji Upendo Isaya amesema: “Biblia inasema tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote ili tufanye uamuzi wa busara, tunahitaji amani ya moyo.”

Viongozi wa dini wakiwa kwenye kongamano la amani lililoratibiwa na kamati ya amani mkoani Mwanza.

Amesema kura ni mkataba kati ya mwananchi na kiongozi, akisihi kuelekea kwenye uchaguzi japo yamesikika mengi lakini kubwa itafutwe amani kwa kufanya uamuzi wa busara.

“Kumbuka hii ni haki yetu ya kikatiba kwa kila Mtanzania ambaye tunatakiwa tuifanye kwa kuchagua yule ambaye tutafanya mkataba naye,” amesema Mchungaji Upendo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Mkoa wa Mwanza, Amina Masenza amewataka vijana na wanawake kutimiza wajibu wao wa kupiga kura bila vurugu, akieleza watu wenye umri kuanzia miaka 18 wanapaswa kushiriki uchaguzi kwa amani.

Mshauri wa kamati hiyo Mkoa wa Mwanza, Dk Jacob Mutashi amesema viongozi wa dini ni washirika wa Serikali katika kulinda amani na kuwataka viongozi wa dini kuwahusia waumini wasikilize maelekezo ya Jeshi la Polisi wanapoenda kupiga kura.

“Amani na utulivu ni ajenda yetu kwenye nyumba za ibada na wakati huu wa uchaguzi tunaweka mkazo kabisa na kusisitiza.

“Tuwaambie watu wetu wasikilize kwa makini maagizo yanayotoka ofisi za polisi kwa sababu siku hiyo ndio watakaokuwepo wakizunguka kila sehemu kutafuta wahalifu,” amesema.

Waziri wa zamani, Lazaro Nyalandu amesisitiza Watanzania kuishi maisha ya utulivu na amani bila ubaguzi wa aina yoyote ili nchi ibaki kuwa kimbilio la wanaohitaji hifadhi.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema mkoa huo uko salama kuelekea uchaguzi mkuu dhidi ya maadui wa usalama wenye mpango wa kuchafua nchi.

“Mwanza kupo salama, Serikali ya Mkoa wa Mwanza na vyombo vya usalama na ulinzi vya mkoa huu tumejipanga ipasavyo kuhakikisha nchi yetu inaingia na kumaliza huu mchakato wa kuchagua viongozi kwa salama na amani,” amesema.