Waliojaribu kumteka mfanyabiashara Tarimo, jela miaka saba

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, iliyopo Kinondoni, imemuhukumu, Fredrick Nsato na wenzake watatu, kifungo cha miaka saba gerezani kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kumteka, mfanyabiashara Deogratius Tarimo.

Mbali na Nsato ambaye ni Wwkala wa mabasi Stendi Kuu ya Mabasi (Magufuli Terminal) iliyopo Mbezi na washtakiwa wengine waliohukumiwa kifungo hicho ni Benki Mwakalebela(40) ambaye pia ni wakala wa mabasi wa Stendi Kuu ya Magufuli Terminal;  Isack Mwaifuani (29) na Bato Tweve (32).

Pia, mahakama hiyo imewaachia huru washtakiwa wawili ambao ni Nelson  Elimusa (24) ambaye ni dereva wa taksi na Anita Temba (27) baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kudhibitisha mashtaka dhidi yao.

Katika kipande cha picha mjongeo kilichosambaa mitandaoni Novemba 11, 2024 kilionyesha watu wakijaribu kumbeba mfanyabiashara huyo wakitaka kumuingiza katika gari lao, huku yeye (Tarimo) akipiga kelele za kuomba msaada akidai kuwa anatekwa.

Na kutokana na uzito wa mwili wake, watu hao walipata upinzani mkali  kutoka kwake katika jaribio la kumbeba na kumuingia katika gari lao na baada ya watu kukusanyika eneo hilo, walimuacha na kukimbia katika eneo hilo.

Kutokana na tukio hilo Desemba 6, 2024, watuhumiwa sita walipandishwa kizimbani mahakamani hapo wakidaiwa kuhusika na tukio hilo na wakasomewa shtaka moja la kujaribu kumteka mtu.

Lakini baada ya usikilizwaji wa kesi hiyo kukamilika mahakama hiyo katika jukumu yake imewatia hatiani washtakiwa wanne na kuwaachia huru wawili.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu, Oktoba 20, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Ramadhani Rugemalira, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.

Hakimu Rugemalira alisema mahakama imewatia hatiani washtakiwa wanne kati sita kama walivyoshtakiwa.

Hakimu Rugemalira alisema upande wa Jamhuri umethibitisha mashtaka pasi na kuacha shaka kwa washtakiwa wanne kati sita walioshtakiwa katika kesi hiyo, baada ya kupeleka mashahidi 15 na vielelezo tisa.

“Mahakama baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri pamoja na utetezi wa washtakiwa hawa, imewatia hatiani washtakiwa wanne kati ya sita walioshtakiwa katika kesi hii” alisema hakimu Rugemalira na kuongeza

” Hivyo, Mahakama inawahukumu, Nsato, Mwaifuani, Mwakalebela na Tweve kifungo cha miaka saba gerezani kila mmoja ili iwe fundisho kwa wengine na haki ya kukata rufaa ipo wazi, iwapo hamjaridhika na uamuzi huu” amesema Hakimu Rugemalira

Awali kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Daisy Makakala amesema pamoja na kuwa  hana kumbukumbu za makosa ya nyuma ya watuhumiwa, lakini anaiomba mahakama itoe adhabu sawa na kifungu walichoshtakiwa ili jamii ijue wanaotenda vitendo vya utekaji siyo Jeshi la Polisi, bali ni watu wa kawaida.

“Naomba mahakama iwape adhabu kali washtakiwa kwa sababu vitendo vya utekaji vimeshamiri sana nyakati hizi, hali inayopelekea Jeshi la Polisi kulaumiwa kwa utekaji huo,” amesema Wakili Makakala na kuongeza.

“Hawa watuhumiwa wangefanikiwa kumkamata Deogratius Tarimo akapotea asionekane … Jamii ingeamini ni Polisi ndiyo wamempoteza hasa na vile wakati wanamkamata walikuwa wakijitambulisha kama Askari Polisi toka Kituo cha Gogoni wakati wakijua ni uongo. Hivyo ili kutoa fundisho kwa hawa watuhumiwa waliokutwa na hatia na jamii yote kwa ujumla mahakama iwape adhabu kali.

Kwa upande wao washtakiwa wao waliomba wapunguziwe adhabu na kudai kuwa wao walikuwa wanasaidia kumteka tu baada ya rafiki yao Frederick kuwaomba wamsaidie kumteka, kwa madai kuwa wanahisi Deo alitembea na mke wa rafiki yake Fredrick.

Washtakiwa kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na shtaka moja la kujaribu kuteka mtu isivyo halali kinyume na vifungu vya 380(1) na 381(1) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Fredrick na wenzake walitenda kutenda kosa hilo Novemba 11, 2024 eneo la Kiluvya Madukani Lingwenye, lllilopo Wilaya ya Ubungo.

Ilielezwa siku hiyo ya tukio katika eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja walijaribu  kumteka mfanyabiashara Deogratius Tarimo kwa nia ya kumuweka kizuizini isivyo halali.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walipandishwa kizimbani mahakamani hapo, Desemba 6, 2024 na kusomewa shtaka hilo.