WANNE KATI YA SITA WALIOJARIBU KUMTEKA MFANYABIASHARA TARIMO BAR JELA MIAKA SABA

VIJANA wanne waliojaribu kumteka mfanyabiashara Deogratus Tarimo wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka saba gerezani baada ya upande wa mashataka kuweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kwamba washtakiwa walitenda kosa hilo huku ikiwachia huru wawili

Vijana hao waliohukumiwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Kinondoni ni askari Fredrick Nsato (21) Mkazi wa Kibamba, Bondia Isaack Mwaifuani (29) Mkazi wa Kimara, Benk Mwakalebela (40) Wakala wa Mabasi katika Stendi ya Magufuli na Bondia Bato Twelve(32) anayeishi Kimara Bonyokwa.

Walioachiwa huru ni Dereva teksi Nelson Msela (24) na Anitha Temba (27), baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao kama walihusika na tukio hilo.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu Ramadhani Rugemalira ameema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka, vielelezo na utetezi wa washtakiwa, ameona kuwa upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha bila kuacha shaka lolote kwa washtakiwa wanne kati ya sita.

“Washtakiwa waliyotiwa hatiani ni Fredrick Nsato, Benki Daniel, Bato Tweve, Isaack Mwaifuani na Mahakama inawaachia huru mshtakiwa watano na sita, Nelson na Anitha,”amesema Hakimu Rugemalira

Akifafanua adhabu hiyo, Hakimu Rugemalira amesema awali washtakiwa walikuwa wakishtakiwa kwa kosa la utekaji, lakini wanahukumiwa kwa kosa la kujaribu kuteka kwa sababu ushahidi wote unaonesha Tarimo aliachwa eneo la tukio.

“Washtakiwa wote wanne mnahukumiwa kifungo cha miaka saba jela kila mmoja kwa kujaribu kumteka mfanyabiashara Deogratus Tarimo, kwa sababu Jamhuri hawa kuthibitisha kama alitekwa, mazingira ya ushahidi walikuwa kwenye harakati ambazo hazikufanikiwa,”amesema

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, upande wa Jamhuri waliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa mujibu wa sheria na iwe fundisho kwa washtakiwa na kwa jamii kwa ujumla.

Hata hivyo, mshtakiwa wa kwanza Nsato alivyopewa nafasi ya kujitetea aliiomba mahakama impunguzie adhabu, kwani ana familia inayomtegemea.

Washtakiwa wengine, waliomba wapunguziwe adhabu kwa madai kwamba mshtakiwa wa kwanza Nsato ambae ni askari aliwadanganya kwamba wakamsaidie kumkamata mtuhumiwa, wao walienda kama raia wema, kwa hiyo walitenda kosa bila kujua.

Katka kesi hiyo Ilidaiwa kuwa Novemba 11,2024 eneo ya Kiluvya Madukani Lingwenye , Wilaya ya Kinondoni , Dar es Salaam washtakiwa walimteka nyara mtu aitwaye Deogratius Talimo lengo la kumdhuru mwili wake.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa namba sita Anitha maarufu kwa jina la Jack ndiye aliyetumika kumlengesha na kumshawishi Tarimo ili atekwe na vijana hao kwa kumdanganya kuwa wakutane kwenye hoteli kwa ajili ya kuzungumza biashara.

Ilidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, Anitha alimpigia simu Tarimo saa saba mchana kumsisitiza kwamba yeye atakuwepo kwenye eneo hilo la hoteli saa nane mchana.

Tarimo alipofika eneo hilo alimpigia simu nakumueleza ameshafika, Anitha akamwambia yeye hayupo aende akasubirie kwenye kaunta ya baa hiyo na mlalamikaji alifanya hivyo.

Baada ya dakika chache baada ya kufika kwa Tarimo katika eneo hilo, mshtakiwa Mwaifuani, Mwakalebela na Twelve walifika eneo na gari ya Toyota Raum namba T 237 EGE wakapaki nje ya geti la hoteli hiyo na dereva ambae hakukamatwa.