WAPIGAKURA 62,207 WATARAJIWA KUPIGAKURA HANDENI MJINI OKT.29

Augusta Njoji na Job Karongo, Handeni TC

ZIKIWA zimesalia siku tisa Watanzania kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Handeni Mjini, Amina Waziri, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kutimiza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo jimboni hapo, Amina amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika na vituo vyote vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.

Amefafanua kuwa wananchi watapiga kura katika vituo walivyojiandikishia, na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeweka utaratibu wa kuhakikisha kila mpigakura anapata fursa ya kupiga kura kwa wakati bila misururu mirefu.

“Tume imejipanga vizuri kuhakikisha wananchi wanapiga kura kwa wakati na kuendelea na shughuli zao za kila siku bila usumbufu. Tunahakikisha utulivu, amani na ufanisi katika mchakato mzima wa upigaji kura,” amesema Amina.

Aidha, amebainisha kuwa mpigakura aliyepoteza kitambulisho chake cha kupigia kura ataruhusiwa kupiga kura kwenye kituo alichojiandikishia kwa kutumia kitambulisho cha Taifa (NIDA), leseni ya udereva, au hati ya kusafiria yenye jina linalofanana na lile lililokuwa kwenye kitambulisho cha kupigia kura.

“Kutokwenda kupiga kura ni kutotimiza haki ya kikatiba. Shime wananchi wa Handeni Mjini mjitokeze kwa wingi kupiga kura. Tume imejipanga kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa amani, utulivu na ufanisi,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Amina, jumla ya wapigakura 62,207 wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo katika vituo 166 vilivyogawanyika kwenye kata 12 za Halmashauri ya Mji wa Handeni.