Wasichana 2,700 wanusurika kukeketwa Mara ndani ya miaka minane

Butiama. Zaidi ya mabinti 2,700 wamenusurika kukeketwa mkoani Mara katika kipindi cha miaka minane iliyopita baada ya kuokolewa na kituo cha kuhifadhi mabinti cha nyumba salama cha Hope For Girls and Women mkoani humo.

Takwimu hizo zimetolewa Wilaya ya Butiama mkoani Mara leo Oktoba 20, 2025 na Mkurugenzi Msaidizi wa Kituo hicho, Domina Mabobe wakati wa uzinduzi wa majengo ya kituo hicho yaliyojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Poland kupitia shirika lake la msaada la Polish Aid.

Mabobe amesema mabinti hao wamenusurika kukeketwa baada ya kufanikiwa kukimbia na kuhifadhiwa kituoni hapo kuanzia mwaka 2017 hadi sasa.

“Hawa mabinti ni wale ambao wazazi au walezi wao walikuwa tayari wamewaandaa kwa ajili ya ukeketaji kwa misimu tofauti katika kipindi hicho na kutokana na jitihada mbalimbali za watu, tumeweza kuwanusuru kufanyiwa kitendo hiki cha ukatili na hili limewezekana kwa sababu tuna sehemu ya kuwahifadhi,” amesema.

bilioni,Balozi wa Poland nchini Tanzania, Sergiusz Wolski, akisaini kitabu cha wageni baada ya kuzindua majengo ya kituo cha nyumba salama cha Hope for Girls cha kilichopo wilayani Butiama Mkoa wa Mara.  Picha na Beldina Nyakeke

Amesema lengo la kuanzishwa kwa kituo hicho ni kuwasaidia mabinti kuepuka kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuwapatia hifadhi salama, huku wakiwezeshwa kuzifikia ndoto zao kwa kupatiwa fursa mbalimbali ikiwepo kurejeshwa shuleni.

Amesema kituo hicho mbali na kuwapa hifadhi mabinti hao, pia, kinatoa mafunzo ya ufundi stadi sambamba na kutoa msaada wa kisheria kwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Rhobi Samuel amesema wamedhamiria kupambana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na wasichana ili kutoa fursa sawa katika jamii katika masuala ya maendeleo, uchumi na kijamii mkoani Mara.

“Kukamilika kwa majengo haya ni hatua kubwa kwetu kwani kutaboresha zaidi utendaji kazi wetu pia eneo hili litakuwa salama zaidi kwa sababu mabinti sasa watakuwa na sehemu salama ya kulala tofauti na awali ambapo tulikuwa hatuna hata uzio,” amesema.

Amesema ni wajibu wa wadau wote kwa pamoja kuhakikisha suala la usawa kijinsia linapaswa kupewa kipaumbele ili wasichana na wanawake wote wapewe fursa sawa za kimaendeleo.

Akizungumza baada ya kuzindua majengo hayo yaliyogharimu zaidi ya Sh1.5 bilioni, Balozi wa Poland nchini Tanzania, Sergiusz Wolski amesema ukatili wa kijinsia ni changamoto inayowakabili wanawake duniani kote, hivyo inahitajika jitihada za pamoja kukabiliana nalo.

“Ukatili wa kijinsia sio hapa Tanzania pekee bali ni tatizo la dunia nzima  na tunatakiwa kuwa na ushirikiano kwa wadau wote yaani Serikali, mashirika na wanaharakati ili kuhakikisha wanawake na wasichana wanaondokana na vitendo hivi vya ukatili,” amesema.

Balozi Wolski amesema Serikali yake imeamua kusaidia kutekeleza mradi huo kutokana na umuhimu wake katika ustawi wa jamii hususani wasichana na kwamba wanaamini kuwa kituo hicho kitakuwa na mchango chanya katika suala zima la haki za wasichana na wanawake.

“Serikali ya Poland kupitia shirika lake la Polish Aid linatoa msaada kwa miradi mbalimbali lakini sio kila mradi tunasaidia ili tusaidie lazima tufanye upembuzi wa kutosha ili tujiridhishe juu ya faida za mradi husika na baada ya kujiridhisha hatukusita kutoa msaada huu,” amesema.

Baadhi ya mabinti wanaohifadhiwa kituoni hapo wameiomba jamii kuachana na vitendo vya ukatili dhidi ya wasichana na wanawake kwa maelezo kuwa vitendo hivyo vinawaathiri kwa kiwango kikubwa.

“Vitendo vya ukatili sasa basi, tunaomba jamii ibadilike, ukeketaji una madhara makubwa kwetu, tumechoka vitendo hivi tunataka kuishia kwa huru na haki, sisi ni binadamu tunastahili kupata haki zetu,” amesema Mary Sabato.

Mradi wa ujenzi wa majengo ya kituo hicho umehusisha ujenzi wa jengo la utawala mabweni mawili yenye uwezo wa kulaza wasichana 160, madarasa mawili, uzio, bwalo na kiwanja cha mpira wa pete kwa gharama ya zaidi ya Sh1.5 bilioni.