‘Askari’ wasiokuwa na viatu wanavyozisaka kura za OMO Zanzibar

Pemba. Mikakati ya ushindi wa nafasi ya urais visiwani Zanzibar kwa Chama cha ACT -Wazalendo, inabebwa na mbinu mbili za kuzitafuta kura za kutosha na kuulinda ushindi kupitia mawakala.

Kwa mujibu wa chama hicho kilichomsimamisha mgombea urais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman jukumu la kuzisaka kura hizo limeachwa mikononi mwa timu maalumu zilizopewa jina la OMO.

Makamu mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Ismail Jussa, anasema timu hizo zilizoanza kazi kabla ya kampeni, zinaendelea kuzisaka kura hadi sasa wakati kampeni zikielekea dakika za lala salama.

Jussa ambaye ni Mwenyekiti wa Timu ya Ushindi Zanzibar, anasema hayo wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi kuhusu mikakati ya ACT-Wazalendo kumtafutia kura Othman maarufu OMO.

Miongoni mwa mikakati walioiweka ni kuimarisha safu za viongozi wa chama hicho, kwa kuzigeuza kamati za uongozi wa ACT –Wazalendo za mikoa, majimbo na matawi kuwa timu za ushindi za chama.

“Tumezibadililisha katika majukumu yake ya kawaida kutoka kamati za uongozi kuwa timu za ushindi wa chama, tumewajengea uwezo wa kuingiza watu wengine wanaoweza kusaidia katika maeneo yao.

“Kazi yao kutoa uongozi na kusimamia mikakati katika maeneo yao. Lakini pili tumeunda timu OMO za ngome za vijana, wazee na wanawake, zinazofanya kazi za kutafuta kura za Othman Masoud ili awe Rais wa Zanzibar,” anasema Jussa.

Jussa anasema timu OMO hizo zilizopo Pemba na Unguja, kwa lugha ya kikampeni duniani wanaitwa askari wasiokuwa na viatu, akisema ndio wanaochanja mbuga.

“Hawa ndio wanaokwenda kufanya kampeni nyumba kwa nyumba, wanawanafuata watu wa makundi yao husika kumuombea kura OMO. Vijana wanakwenda kwa vijana wenzao, wanawake wanakwenda kwa wanawake wenzao.

“Vivyo hivyo kwa upande wa ngome ya wazee wanaokwenda kwa wazee wenzao. Hizi timu OMO zinatoka katika majimbo yote 50 yaliyopo Pemba na Unguja,” anaeleza Jussa.

Jussa anasema majimbo 32 ya Unguja, yana timu OMO, na 18  Kisiwa cha Pemba.

Anaeleza kuwa jambo jingine linalowapa faraja ni kwamba, Othman ataibuka kidedea katika uchaguzi wa Oktoba 29, ni chama hicho kufanya kampeni bila kuacha kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

“Tumefanya mikutano yote ukiondoa mmoja tumeuacha kutokana kifo cha Abass Mwinyi (mgombea ubunge wa Fuoni-CCM). Karibu majimbo yote tumeyafikia ili kumnadi na kumuombea kura OMO,” anasema Jussa.

Juzi, akihutubia mkutano wa hadhara wa Othman uliofanyika Uwanja wa Ole Kianga Laurent Mkoa wa Kusini Pemba, Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Zanzibar Omar Ali Shehe alisema kati ya mikutano ya majimbo ya 36, tayari 33 wameyafikia

“Tutakuwa tumebakiwa na mikutano mitatu, tutakwenda Chambani, kisha Tumbe na tutamalizia Wete(Pemba) tutakapofunga dimba. Kati ya majimbo 50, Ole ni jimbo la 47, kati ya majimbo 18 ya Pemba, hili jimbo la 15,” alisema.

 “Safari yetu ya kampeni ipo ukingoni, lakini tunaendelea vizuri na kumekuwa na mafanikio makubwa. Wito wangu kwa upande wa pili, wajiandae kufanya kazi na Othman, tena ikiwezekana waanze sasa hata kuimpigia simu wajiandae kisaikolojia, wimbi hili halizuiliki,” alidai Shehe.

Hata hivyo, Jussa anasema mbali na mikutano ya hadhara ambayo imekuwa na mafanikio makubwa ikiwamo kuelezea ilani, pia Othman amekuwa akifanya vikao vinavyohusisha makundi mbalimbali, kila siku ya kampeni zake.

“Kabla ya kuanza mikutano ya kampeni, Othman nyakati za asubuhi hadi mchana amekuwa akikutana na makundi ya wakulima, wavuvi, wafanyabiashara, wafugaji, wajasiriamali, vijana, wanawake na wananchi,”anasema.

“Pia, Othman anatembelea masoko na kuzungumza na wananchi, viongozi wa kidini na watu walioathirika na changamoto mbalimbali ikiwamo kuporwa ardhi zao,” anasema Jussa.

Anasema hatua hiyo imewezesha ACT-Wazalendo kujiweka karibu zaidi na jamii, hatua itakayorahisisha mgombea wa chama hicho kupata kura za kutosha ifikapo Oktoba 29, mwaka huu.

Katika mikakati ya kulinda ushindi wa chama hicho, Jussa anasema wameweka mawakala kila kituo cha kupigia kura ili kufuatilia mwenendo wa kura za Othman.

“Tunajua hapa ndipo kwenye changamoto kubwa kwenye masuala ya uchaguzi, lakini ACT-Wazalendo imejidhatiti ili kulinda ushindi wetu na wagombea wetu wote wanatangazwa washindi kuanzia udiwani, uwakilishi, ubunge hadi urais,” anasema. “Narudi tena, hatuna wasiwasi na ushindi wetu, kwa sababu namba hazidanganyi. Kwa mujibu wa kampeni zetu zilizofanyika kisayansi na data zetu, sisi tumeshashinda kazi iliyobaki ni kumaliza kujenga hamasa kujitokeza kupiga kura,” anasema Jussa.

Juzi, Othman akiwaomba kura wananchi wa Ole, alisema ili kufanikisha ushindi ni muhimu kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, mwaka huu akisema silaha pekee ya kuzikabili dosari zinazojitokeza katika uchaguzi ni kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

“Wazanzibari na wana ACT jitokezeni kupiga kura mkiwa na amani pamoja na imani kuwa sisi ni washindi, tunakwenda kuulinda ushindi wetu. Hawa dawa yao moja tu asibakie mtu nyumbani,” alisema Othman.

Kinachowapa jeuri ya ushindi

Katika mazungumzo yake, Jussa anafichua kinachowapa jeuri ya kuibuka ushindi Oktoba 29 ni aina ya mgombea wao waliomsimamisha katika uchaguzi wa mwaka huu.

“Omo anauzika kutokana na historia yake, tofauti na vyama vingine, mtu yeyote mwenye kuzifahamu siasa za Zanzibar, anafahamu ajenda ya Zanzibar ni kupigania masilahi yake na mamlaka kamili.

“Hili, Othman analiweza vizuri na ana historia kubwa sana, kikubwa zaidi kilimjenga ni uamuzi wake wa kutoka nje ya Bunge Maalumu la Katiba (BMK) kitendo kinachokumbukwa na kila mtu,” anasema Jussa.

Mwaka 2014 akiwa mjumbe wa BMK kwa tiketi ya mwanasheria mkuu wa Zanzibar, Othman alitolewa nje ya Bunge hilo, baada ya kutofautiana na msimamo wa CCM, katika baadhi ya vifungu vya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.

Hatua hiyo ilisababisha Othman kuvuliwa wadhifa huo wa uanasheria mkuu wa Zanzibar, chini ya utawala wa Dk Ali Mohamed Shein.

Jussa anaendelea kueleza kuwa, jambo jingine linalowapa jeuri ni Othman kuijua vizuri historia ya Zanzibar nje, ndani jambo linalorahisisha kupata kura zaidi Oktoba 29.

 “Wengi bado wanamkubali Othman na mara tuna ushirikiano mkubwa hadi kutoka chama cha …tuna washirika wengi sana hadi ofisi mbalimbali za Serikali,” anaeleza Jussa.

Jambo jingine Jussa anasema kitendo cha ACT -Wazalendo, kuwasimamisha wagombea waliopitishwa katika mchakato wa kura za maoni kimewasaidia kujenga ushirikiano mkubwa miongoni mwa Wazanzibari katika majimbo mbalimbali.

“Asilimia 95 wagombea wote walioshinda kura za maoni wamepitishwa na kamati kuu, tuliheshimu matakwa ya wajumbe. Jambo hili limeleta utulivu mkubwa ndani ya chama,” anasema Jussa.

Pia, anasema hatua ya ACT – Wazalendo kuonekana hadharani kukemea na kupinga vitendo vya kifisadi na rushwa ni karata nyingine inayowapa jeuri ya kuibuka kidedea.

Kutokana na msimamo huo, Othman kupitia mikutano yake ya kampeni ya Unguja na Pemba, amekuwa akiahidi kuwa akishika madaraka atakwenda kukomesha vitendo hivyo alivyodai viwanyima haki Wazanzibari na kwamba ataisafisha Serikali.