Moshi. Mgombea ubunge wa Moshi Mjini kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Patrick Assenga, ameahidi kuwa endapo atapata ridhaa ya kuwa mwakilishi wa jimbo hilo atarejesha hadhi ya Moshi kama mji safi zaidi barani Afrika.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo Kata ya Mawenzi, Assenga amesema dhamira yake kuu ni kuhakikisha Moshi inarejea katika hadhi yake ya kipekee kwa kuboresha mipango miji, miundombinu, na mazingira ya wafanyabiashara wadogo.
“Nina mpango wa kuimarisha mipango bora ya mji, kuwezesha wamachinga na wafanyabiashara wadogo, kuondoa ushuru na kodi kandamizi, pamoja na kupigania maslahi ya watumishi wa umma na wastaafu,” amesema Assenga.
Mbali na hayo, amesema kipaumbele kingine ni kuboresha miundombinu ya barabara, hasa zile za pembezoni ambazo zimekuwa changamoto hasa kipindi cha mvua ili kurahisisha usafiri na biashara ndani ya jimbo hilo.
Aidha Assenga ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wa Moshi Mjini kuwa makini katika maamuzi yao na kutumia kura zao kuleta mabadiliko.
Amesisitiza kuwa mamlaka ya nchi yapo mikononi mwa wananchi, na hivyo kuwaomba kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi na kuichagua Chaumma.
“Wagombea wote tunakuja kwenu kuomba kura, lakini wenye maamuzi ni ninyi wananchi. Oktoba 29 amkeni mapema, mkapige kura, mkanichague Asenga kuwa mbunge wenu wa Moshi Mjini. Mwaka mmoja tu, nitaleta mabadiliko makubwa,” ameahidi Assenga
Amesema akipewa nafasi ataongoza juhudi za kutunga sheria zitakazowabana mafisadi na kubuni sera zitakazoendana na maisha halisi ya Watanzania.
“Tuache kuwa waoga, tuache kukata tamaa. Dhambi kubwa kuliko zote ni woga na ya pili ni kukata tamaa. Amkeni watu wa Moshi, safari hii tumejipanga vizuri. Nendeni mkapige kura bila hofu, tumalizane na utawala huu,” amesema.
Kwa upande wake mgombea udiwani kata ya Mawenzi, Exaud Mamuya amesema atashirikiana na Assenga kuleta mabadiliko ya kweli katika kata hiyo.