Arusha. Sekta ya Uhifadhi nchini imepata msukumo mpya baada ya Shirika la Uhifadhi Afrika (AWF) kukabidhi mradi wa jengo la Kikosi cha Mbwa Nusa wanaodhibiti utoroshwaji wa nyara za Serikali kwenye viwanja vya ndege wenye thamani ya zaidi ya Sh137 milioni.
Mradi huo umetekelezwa na AWF umelenga kuiwezesha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (Tawa) kutimiza majukumu yake kikamilifu kupitia kitengo chake cha udhibiti na utoroshwaji wa nyara za Serikali kupitia maeneo ya mipakani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tawa, Meja Jenerali mstaafu, Hamis Semfuko akizungumza leo Jumanne Oktoba 21,2025 wakati wa uzinduzi wa mradi huo ameishukuru AWF kwa mchango huo utakaowezesha Tawa kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
“Nachukua fursa hii kutoa shukurani za dhati kwa AWF kwa msaada na mchango wao mkubwa uliowezesha ujenzi wa jengo hili la Kikosi cha Mbwa Nusa katika ofisi ya Kanda ya Kaskazini ,huu ni uthibitisho wa ushirikiano endelevu kati ya Tawa na wadau katika kulinda rasilimali za wanyamapori,
Jengo hili ni muhimu kwa kuwa litawezesha kufanya kazi kwa ufanisi, wote ni mashahidi na tunatambua kuwa wahalifu wamekuwa wakibadili mbinu katika kufanya uhalifu.
“Hivyo matumizi ya mbwa nusa ni nyenzo muhimu na ya kisasa katika kudhibiti uhalifu unaohusiana na usafirishaji haramu wa nyara za Serikali na biashara haramu ya wanyamapori.” amesema Jenerali Semfuko.
Kamishna wa Uhifadhi wa Tawa, Mlage Kabanga amesema Mbwa Nusa wamekuwa wakitumika kubaini nyara kwenye maeneo ya vituo vya forodha vya Namanga, Holili, Tarakea na Horohoro, viwanja vya ndege vya Kilimanjaro na Arusha pamoja na Bandari ya Tanga.

“Kikosi hiki ambacho jukumu lake kuu ni kudhibiti uhalifu wa nyara na biashara haramu ya wanyamapori, kutokana na mashirikiano yaliyopo kati ya Tawa, AWF na kufanikiwa kujenga jengo hili ambalo lina ofisi, sehemu ya kukaa watumishi, hali hii inawezesha kikosi chetu cha Mbwa Nusa kufanya kazi katika mazingira bora na kwa ufanisi zaidi,”amesema Kamishna Kabange.
Naibu Kamishna wa Huduma za Utalii wa Tawa, Leonald Mayeta amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na AWF ilianzisha Kikosi cha Mbwa Nusa mwaka 2015 ikiwa ni sehemu ya juhudi mahsusi za kupambana na ujangili na usafirishaji haramu wa nyara za wanyamapori.
Amesema lengo kuu la kuanzishwa kwa kikosi hicho ni kusaidia kubaini nyara zilizofichwa kama vile meno ya tembo, ngozi na kucha za simba pamoja na magamba ya kakakuona ambazo ni vigumu kugundulika kwa njia za kawaida za ukaguzi.
Kamishna huyo amesema katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2025 doria za kikosi cha mbwa zimefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa wa ujangili 99, meno ya tembo vipande 258 vyenye jumla ya kilogramu 753, kakakuona hai watatu, magamba ya kakakuona 6,000, nyamapori mbichi kilogramu 91, meno ya kiboko yenye uzito wa kilogramu 3.7 na meno ya simba tisa.
Mkurugenzi Mkaazi wa AWF, Pastory Magingi amesema biashara haramu ya wanyamapori bado ni mojawapo ya uhalifu wa kimataifa unaoingiza fedha nyingi duniani, ikiwa ni mapato ya hadi dola za Marekani bilioni 20 kila mwaka.
Amesema kwa mujibu wa CITES, Afrika Mashariki hasa nchi za Kenya, Tanzania, na Uganda zimetambuliwa kwa muda mrefu kama chanzo na njia ya kupitisha meno ya tembo, magamba ya kakakuona na bidhaa nyingine za thamani kubwa za wanyamapori.
“Kwa kutambua changamoto hii, Shirika la AWF kwa kushirikiana na Tawa ilianzisha Mpango wa Mbwa kwa ajili ya Uhifadhi mwaka 2015, lengo la ushirika huu ilikuwa kuimarisha uwezo wa utekelezaji wa sheria kwa kutumia mbwa waliopatiwa mafunzo maalumu,”amesema Magingi.