PAMOJA na kusota benchi, kipa wa Dodoma Jiji, Daniel Mgore amesema anasubiri muda wake ukifika, huku akitoa matumaini kwa timu hiyo kurejesha heshima yake msimu huu na kutamba kushinda leo dhidi ya Mtibwa Sugar.
Kipa huyo ambaye alikuwa tegemeo alipokuwa akikipiga Biashara United, tangu kuondoka kikosini humo misimu minne nyuma amekuwa akisugua benchi alipotua Dodoma Jiji.
Hata hivyo, kwa muda huo kipa huyo amekuwa akikutana na upinzani kwa makipa wenzake kikosini, huku akipita mikono tofauti ya makocha na Melis Medo alionekana kumwamini kabla ya hali kubadilika.

Msimu uliopita, kipa huyo alicheza takribani mechi nne sawa na dakika 360, huku ufalme ukiwa kwa mpinzani wake raia wa DR Congo, Alain Ngeleka na msimu huu, Ally Salim aliyetua kikosini hapo akitokea Simba, ndiye anang’ara.
Dodoma Jiji ambayo leo Jumatano itakuwa nyumbani kuikaribisha Mtibwa Sugar, imecheza mechi nne ikishinda moja dhidi ya Coastal Union 2-0, sare moja na kupoteza mbili, ipo nafasi ya 10, huku wapinzani wakiwa nafasi ya tisa kwa pointi sawa.
Mgore aliliambia Mwanaspoti pamoja na msoto wa benchi anaoupitia, lakini hajakata tamaa badala yake anaendelea kuonyesha kitu mazoezini ili kushawishi benchi la ufundi kumpa namba.
Kuhusu matokeo waliyonayo kwa sasa, amesema si mazuri wala mabaya sana na kwakuwa ligi ndiyo imeanza bado wanayo nafasi ya kupambana kukaa nafasi nzuri kwenye msimamo, akitamba kushinda dhidi ya Mtibwa Sugar.

“Mchezaji yeyote anasajiliwa kucheza, ukikosa nafasi unaweza kupoteza ubora, lakini binafsi sijakata tamaa na ninaendelea kupambana mazoezini ili kushawishi kupata namba.
“Uamuzi upo kwa kocha kutegemea na aina ya mechi na mipango yake nani aanze au kusubiri, nangoja muda ukifika nitaonekana uwanjani, matarajio yetu ni kushinda mechi ya leo,” amesema Mgore.