Darasa la nne kuanza mitihani kesho kwa mtaala mpya

Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza, wanafunzi  milioni 1.6 wa darasa la nne wanatarajiwa kuanza upimaji wa kitaifa Oktoba 22,23 mwaka huu kwa kuzingatia Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 toleo 2023 na mtaala ulioboreshwa.

Wanafunzi hao watafanya mitihani ya masomo sita ambayo ni sayansi yenye hisabati, jiografia na mazingira na upande wa sanaa ni michezo, Kiswahili, Kiingereza na historia ya Tanzania na maadili.

Pia, kutakuwa na uchaguzi wa masomo matatu ambayo ni lugha ya Kichina, Kiarabu na Kifaransa.

Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 21,2025  na Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Profesa Said  Mohamed wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

“Katika usajili huu jumla ya wanafunzi waliosajiliwa kufanya upimaji wa kitaifa ni milioni 1.58 ambapo kati yao wavulana ni 768,290 sawa na asilimia 48.31 na wasichana ni 817,850 sawa na asilimia 51.69,”amesema.

Profesa Mohamed amesema katika takwimu hizo wanafunzi watakaofanya upimaji wa lugha ya Kiingereza ni 106,503 sawa na asilimia 6.7, lugha ya Kiswahili milioni 1.475.

Pia, amesema wanafunzi wenye mahitaji maalumu miongoni mwa wanafunzi hao ni  5,750 ambapo kati yao wenye uoni hafifu ni 1,164 na wasioona 111,wenye uziwi ni 1,161 na wenye ulemavu wa akili 1,641 na wenye ulemavu wa viungo 1,673.

Profesa Mohamed amesema katika upimaji huo, masomo sita pekee ndiye yatatumika kufanyiwa upimaji baada ya kuchaguliwa na wataalamu.

Profesa Mohamed amesema maandalizi yote kwa ajili ya upimaji huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za upimaji pamoja na nyaraka zote muhimu zinazohusu upimaji huo, katika halmashauri na manispaa zote nchini.

“Aidha, maandalizi yote kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu yamefanyika ipasavyo.”

Kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zimefanya maandalizi yote muhimu ikiwa ni pamoja na kutoa semina kwa wasimamizi wa upimaji na kuhakikisha kuwa mazingira ya vituo vya upimaji yapo salama,”amesema.

Profesa huyo amesema kamati za mitihani zimeweka mikakati ya kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu.

Akizungumza umuhimu wa mtihani huo amesema  ni muhimu kwa kuwa huwezesha kufahamu kiwango cha wanafunzi katika kumudu stadi za juu za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.

“Matokeo ya upimaji huu huwezesha wadau wa elimu, wakuu wa shule na walimu kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika maeneo yanayobainika kuwapa changamoto wanafunzi.

“Hivyo, ni upimaji muhimu kwa wanafunzi, wasimamizi wa elimu na jamii nzima kwa ujumla katika Taifa letu,” amesema.