Dk Nchimbi: Tutasogeza huduma za afya karibu zaidi

Songwe. Wakati kampeni za uchaguzi mkuu zikielekea ukingoni, mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema lengo la chama hicho katika kipindi cha miaka mitano ijayo kitahakikisha huduma za afya zinapatikana ndani ya kilomita tano kutoka makazi ya wananchi.

Pia, amesema ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2025/2030 chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inakwenda kutekelezwa kwa kasi ili kuchochea maendeleo ya wananchi.

Dk Nchimbi ametoa ahadi hizo leo Jumanne, Oktoba 21, 2025 katika mikutano aliyoifanya Jimbo la Ileje na Momba, mkoani Songwe, ikiwa ni siku nane zimebaki Watanzania milioni 37.6 waliojiandikisha kupiga kura kuamua nani awe diwani, mbunge na Rais.

Katika mikutano hiyo, Dk Nchimbi amewanadi wagombea ubunge wa maeneo hayo, Godfrey Kasekenya (Ileje), Condester Sichalwe (Momba), madiwani na za urais wa Samia.

Ameeleza mafanikio ya miaka mitano iliyopita kwenye sekta mbalimbali ikiwemo za afya, elimu, uchumi, miundombinu ya barabara na kilimo.

Pia, wanakwenda kufanya nini miaka mitano ijayo endapo watapata ridhaa ya kuendelea kuwatumikia Watanzania.

Dk Nchimbi amesema Serikali ya CCM katika miaka mitano ijayo inakwenda kuanzisha utaratibu wa bima ya Afya kwa Watanzania wote na kusogeza zaidi huduma za afya karibu na wananchi.

“Sisi wote tunataka ndani ya miaka mitano, huduma ya afya ya kila Mtanzania pamoja na kuimarika, lakini kila Mtanzania apate huduma hiyo karibu zaidi.

“Tunataka kila Mtanzania awe na uhakika wa huduma ya afya ndani ya kilomita tano kutoka eneo analoishi,” amesema Dk Nchimbi akiwa Momba.

Ujenzi wa shule za msingi, sekondari, maabara na madarasa kwa shule za zamani, miradi ya maji, kuboresha sekta ya kilimo, barabara za lami na changarawe kujengwa ni miongoni mwa ahadi alizozitoa akiwa Ileje na Momba.

Jambo jingine ambalo Dk Nchimbi amelizungunza endapo watapata ridhaa ni kuimarisha amani na usalama wa nchi yetu.

“Mpaka sasa Rais Samia ameweza kuhakikisha tangu amechukua madaraka miaka minne na nusu iliyopita, nchi yetu ina amani, ina umoja na utulivu, tunakwenda kuviendeleza maana hivyo ndio vitu vya msingi vya kwanza kwa watu wetu wapo,” amesema Dk Nchimbi.

Kwa upande wake, Godfrey Kasekenya amesema Serikali ya awamu ya sita ya Chama cha Mapinduzi imefanikiwa kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wenye gharama ya Sh5 bilioni katika mji wa Itumba na Isongole.

“Mradi huo utakwenda kutatua changamoto ya mradi wa maji ulioikumba miji hiyo tangu kuanzishwa kwa wilaya hiyo miaka ya 1975 ambao ukikamilika utaongeza upatikanaji wa maji kutoka asilima 80 mpaka 90,” amesema Kasekenya.