DK.SAMIA AAHIDI UPATIKANAJI MAJI YA UHAKIKA DAR KUPITIA MRADI WA BWAWA LA KIDUNDA

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.Samia Suluhu Hassan amesema katika miaka mitano ijayo Serikali itaendelea kukamilisha utekelezaji wa mradi wa bwawa la Kidunda lenye thamani ya Sh bilioni 336 litakalohudumia mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Dk.Samia amesema hayo leo Oktoba 21,2024 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kinondoni na Ubungo jijini Dar es Salaam akiwa katika mkutano wa kampeni kuomba kura kuelekea Oktoba 29 mwaka huu.

“Mradi wa wa pili tunaokwenda kufanya ili kuondoa uhaba wa maji Dar es Salaam  hasa wakati wa kiangazi  ni mradi mkubwa wa kutoa maji katika mto Rufiji ambao kazi ya upembuzi yakinifu na utafiti wa kina tayari tumekwishaianza.

“Na awamu  hii tunakwenda kufanya utekelezaji ili  Dar es Salaam ipate maji kutoka Kidunda, Ruvu na mto Rufiji kuondoa kabisa kadhia ya uhaba wa maji,”amesema Dk.Samia alipokuwa akielezea mikakati ya Serikali katika miaka mitano ikayo katika kutatua changamoto ya uhaba wa maji kwa baadhi ya maeneo.

Kwa upande wa migogoro ya ardhi Dar es Salaam hasa maeneo ya Mabwepande, Mbezi, Bunju na Nyakasanga amesema Serikali ya mkoa na wilaya zinaendeela na jitihada za utatuzi kuimaliza.

Amefafanua kuwa kwa ujumla wamepanga kwenda kuongeza nguvu kwenye utatuzi wa migogoro na urasimishaji wa maeneo ya makazi.

Katika hatua nyingine Dk.Samia amezungumzia  makundi maalum ambapo ameeleza kuwa Serikali inatekeleza matamko ya kimataifa yakiwemo tamko la Milenia na tamko la Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Amesema kuwa matamko hayo yanaitaka serikali kutokumuacha nyuma mwanadamu yeyote.”Kwasababu hizo Serikali imechukua hatua maalum kutekeleza mipango mbalimbali kwa watu wenye ulemavu.

“Hata kwenye mageuzi yetu ya elimu tumewawekea mpango wao, mageuzi ya afya tumewawekea mpango wao, mambo ya kutafuta huduma kwenye nyumba za serikali tumewawekea mpango wao.

“Tumekwenda na matamko ya kimataifa yakutokumuacha mtu nyuma, hivyo ndivyo tunavyotekeleza,” amesema Dk.Samia.