Unguja. Rais mstaafu wa awamu ya saba wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameongoza mamia ya waombolezaji kumzika Mussa Aboud Jumbe katika makaburi ya familia, Migombani Unguja, Zanzibar
Mussa ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Rais wa awamu ya pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, ambaye amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Oktoba 21, 2025 katika Hospitali ya Mnazimmoja alipokuwa akipatiwa matibabu.
Akitoa shukurani kwa waombolezaji baada ya maziko, msemaji wa familia, Mustapha Aboud Jumbe amesema Mussa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kupumua kwa kipindi kirefu, alipelekwa India mara mbili kwa ajili ya matibabu.
“Alikuwa na matatizo ya pumzi amekwenda India mara mbili, lakini amefia katika chumba cha wagonjwa mahututi Hospitali ya Mnazimmoja,”
Amesema, “imebidi tuyaseme haya maana yasije kuibuka mengine kwenye mitandao yakasemwa ambayo siyo.”
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa familia, Mussa ameacha wajane wawili na watoto 12, mdogo kabisa akiwa na miezi mitatu. Kati ya hao watano ni wa kiume na wa kike saba.
“Tumemzika hapa kwani hata wazee wetu baba na mama na dada zetu wamezikwa hapa,” amesema.
Mustapha amesema, Mussa ambaye amefariki dunia akiwa na miaka 58, alikuwa ni mtoto wa mwisho katika familia hiyo.