Unguja. Mwenyekiti wa Kigoda cha Karume, Eginald Mihanjo amesema kukosekana vyuo vinavyotoa mafunzo ya uongozi ndio chanzo cha kupata viongozi wasiokuwa na maadili na kufuata misingi bora wanapopata nafasi hizo.
Hayo ameyasema leo Jumanne Oktoba 21,2025 wakati wa Kongamano la kitaaluma na uzinduzi wa hifadhi ya kidijitali ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Taifa (Suza).
Amezitaka mamlaka kuweka vyuo vinavyotoa mafunzo kwa lengo la kupata viongozi wenye maadili na wanaofuata misingi bora wanapopata nafasi za kuongoza.
Amesema, tatizo la uongozi halikuanzia kwa rika ya kwanza ya Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Zanzibar badala yake lilianzia katika rika la pili tangu kufutwa kwa vyuo vya uongozi mwaka 1990.
“Mara nyingi nawaambia wenzangu msiwalaumu viongozi kwani viongozi wote waliopo hawajapata mafunzo na huo ndio ukweli kwa sababu vyuo vilifungwa hivyo wanalaumiwa nini? Amehoji.
Ameongezea kuwa, “Ikiwa hatuwezi kuwaandaa viongozi wa rika la tatu itakuwa tatizo kubwa sana na ukoloni utarudi, tunapaswa kuonesha njia ya namna ya kuelekea mbele na kuzalisha viongozi hao”, amesema
Mwenyekiti huyo, amesema bila ya kuwa na mwongozo maalumu hayo yote hayatofanikiwa hivyo ametoa wito kwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akipata nafasi ya kurudi madarakani awamu ya pili aweke mazingira mazuri kwa rika ya tatu ili Tanzania iwe salama.
Mwenyekiti huyo, amesema Kigoda hicho kinapaswa kuwa chombo cha ukombozi wa Afrika kwa kuendeleza maono na fikra za waasisi, kwani tatizo la Afrika ni ombwe la uongozi na anashangazwa kuona tatizo hilo linaendelea kuota mizizi.
Amefafanua kuwa, kiongozi bora ni yule ambaye anaweza kutatua matatizo ya watu ili kuwa na Taifa salama kinyume na hapo huyo sio kiongozi.
Akitoa mada katika kongamano hilo, Profesa Patrick Lumumba amesema Kigoda hicho kinatakiwa kuendeleza siasa za maadili kwani kukosekana kwa jambo hilo ndio sababu ya viongozi wa Afrika kuuwana kwa lengo la kupata madaraka.
Amesema, hali hiyo inachangiwa kwa kutokuwa na mifumo mizuri yenye maadili na mustakabali wa mataifa yao ndio maana wana kiu ya kuongoza kila siku.
Vilevile, amesema kwa sasa wasomi ni wengi lakini hawana maono ya kuongoza ndio maana wanategemea tafiti ambazo hazileti maendeleo ya nchi.
Amesema, hayati Karume hakusoma sana lakini alikuwa na maono ya kufanya maendeleo yaliyodumu vizazi hadi sasa.
Pia, amesema demokrasia ni mapambano ya hoja na sio dini na ukabila ndio maana vijana wanapaswa kuuliza maswali ya msingi yanayotafsiri maono yanayolenga kutatua matatizo ya wananchi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Suza, Profesa Moh’d Makame Haji amesema uzinduzi huo ni chombo muhimu cha maarifa na utafiti katika kujifunza kupata viongozi wenye maadili na wazalendo wa nchi.
Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohamed Mussa amesema mapambano ya Rais Karume hayakuwa ya silaha pekee, bali yalikuwa yakuhamasisha mshikamo kwa wananchi kwa sababu alitambua Afrika ndio mwongozo wa ukombozi wa nchi. “Ndio sababu ya kuungana kwa kuondoa tofauti za kiuchumi za kikabila ambazo hapo awali ziliwagawa wananchi wa Zanzibar.”