Kamwe ataja siku ya kutua kocha mpya Yanga

BAADA ya kuondoka kwa kocha wa Yanga, Romain Folz, Meneja Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe amesema ndani ya siku tatu kocha mpya atakuwa ameshatua.

Oktoba 18, 2025 muda mchache baada ya Yanga kupoteza ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya Silver Strikers katika mechi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya pili, ilitangaza kuachana na Folz.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kamwe alisema, kuna uwezekano mkubwa mpaka kufikia siku ya mechi ya marudiano Jumamosi wiki hii, kocha mpya atakuwa ameshatua Dar es Salaam.

Amesema kuwa, Yanga tayari imeshaingia kambini leo Oktoba 21, 2025 saa 6:00 mchana, chini ya kocha msaidizi Patrick Mabedi ambaye ndiye atasimamia mechi hiyo.

“Wakati wowote ndani ya siku hizi tatu kocha mpya atakuwa ameshafika mjini, lakini mpaka sasa Mabedi ndiye atakuwa kocha atakayesimamia mchezo huo.

KAM 01

“Yanga chini ya Mabedi iko kwenye mikono salama, tunamuamini na mechi hii ya nyumbani basi tuna uhakika kwamba tutakwenda kupata burudani na ushindi,” amesema Kamwe.

ISHU YA MECHI
Ally amesema kuwa, mechi hiyo itakuwa haina kiingilio kwani mashabiki walituma maombi kwa viongozi wa klabu hiyo kwamba waingie bure ili kujaza uwanja na kuwapa morali wachezaji.

Alisema yapo maeneo ambayo yatakuwa rasmi kwa wageni ikiwemo VIP A na B, hivyo mashabiki wakae pengine kote kasoro huko.

“VIP A na B itakuwa kwa wageni maalum, ila kwa mashabiki wataingia na kukaa kokote ukiachana na maeneo hayo bure kabisa.

YANG 04

“Hili ni ombi ambalo viongozi wamelipokea kutoka kwa mashabiki na ilitolewa ahadi kwamba watakwenda kujaza uwanja na wachezaji wameahidi kwamba wataivusha timu hatua ya makundi,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Kwa wale wenye dhamira mbaya na mchezo huo basi usifike kabisa uwanjani ila kama wewe ni shabiki basi njoo utulie uangalie mechi, kwani hiyo siku tunakwenda kupambania heshima ya Yanga, kwa hiyo isitoke mtu akaharibu.”

Yanga inashuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar Jumamosi Oktoba 25 dhidi ya Silver Strickers ya Malawi, ikiwa na rekodi ya kupoteza ugenini. Inahitaji kushinda kwa angalau tofauti ya mabao 2-0 ili kufuzu makundi.