Lugha ya alama ni chombo muhimu cha mawasiliano kinachowezesha watu wenye ulemavu wa kusikia, kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii, kielimu na kiuchumi.
Ni lugha kamili yenye sarufi, misamiati na kanuni zake, sawa na lugha nyingine za mazungumzo.
Kwa wasiosikia, lugha ya alama ndiyo daraja linalounganisha ulimwengu wao na jamii pana, ikiwapa uwezo wa kueleza mawazo, hisia na maarifa kwa uhuru na heshima.
Hata hivyo, licha ya umuhimu wake, ufundishaji, ujifunzaji na matumizi ya lugha ya alama shuleni na vyuoni bado ni changamoto.
Walimu wachache wamepata mafunzo rasmi ya kufundisha kwa kutumia lugha ya alama, na vifaa vya kujifunzia bado ni haba.
Hali hii imechangia kundi kubwa la wanafunzi wasiosikia kukosa usawa wa kielimu, jambo linalowaweka katika hatari ya kutengwa na kupoteza fursa muhimu za maendeleo.
Kwa upande mwingine, jitihada za Serikali, vyuo vya elimu ya juu, na taasisi zisizo za kiserikali zinaendelea kuibua matumaini mapya. Programu za mafunzo ya walimu wa lugha ya alama, tafsiri ya nyaraka za kielimu kwa alama, na uhamasishaji wa jamii kuhusu haki za watu wenye ulemavu, zimeanza kuonyesha mwanga, ingawa bado zinahitaji nguvu na uratibu mpana.
Makala haya yanachambua nafasi ya lugha ya alama Tanzania, ikitazama changamoto zilizopo, juhudi zinazofanyika, na mapendekezo ya hatua za kuchukua, ili kuhakikisha elimu inapatikana kwa usawa kwa watoto wote wakiwemo wenye ulemavu wa kusikia.
Kupitia mjadala huu, tunatafakari kama taifa limepiga hatua ya kutosha katika kuhakikisha kaulimbiu ya “elimu kwa wote” inakuwa halisi, si kwa nadharia tu bali pia kwa vitendo.
Wadau wa elimu, watafiti na walimu wanakiri kuwa pamoja na jitihada za Serikali, lugha hii haijapewa uzito unaostahili kulingana na nafasi yake katika kukuza haki ya elimu kwa wanafunzi viziwi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekolojia, nchi inakadiriwa kuwa na zaidi ya wanafunzi 16,000 wenye changamoto ya kusikia, wanaosoma katika shule za msingi na sekondari.
Hata hivyo, idadi ya walimu wenye ujuzi rasmi wa lugha ya alama ni ndogo sana ukilinganisha na mahitaji halisi.
Hili linaifanya elimu kwa wanafunzi viziwi kuwa changamoto kubwa, licha ya uwepo wa sera nzuri za elimu jumuishi.
Vyuo vya elimu vinavyoibeba lugha ya alama
Dk Justin Msuya, Mhadhiri kutoka Kituo cha Taaluma za Mawasiliano, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema vyuo vichache tu nchini vinatoa kozi zinazohusisha lugha ya alama, na hata hivyo, nyingi hazilengi moja kwa moja kuwaandaa walimu wa kufundisha viziwi.
“Hata pale tunapofundisha Lugha ya Alama ya Tanzania, wanafunzi wetu wengi ni wa masomo ya Language Studies na siyo walimu watarajiwa,” anasema Dk Msuya.
Anaongeza: “Programu za astashahada za lugha ya alama zipo, lakini zinalenga zaidi wakalimani na si walimu wa kufundisha shuleni.”
Anataja vyuo kama Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine – Tawi la Tabora (AMUCTA) na Chuo cha Ualimu Patandi mkoani Arusha kama taasisi zinazoongoza katika kutoa walimu wa elimu maalum wanaojifunza lugha ya alama kwa ajili ya kufundisha watu wasiosikia.
Licha ya jitihada hizo, Dk Msuya anasema kuna changamoto kubwa ya uhaba wa wataalamu, tafiti chache, na upungufu wa vifaa vya kufundishia, hali inayozuia maendeleo ya lugha hiyo kitaaluma.
“Ufundishaji wa lugha ya alama ni tofauti na lugha nyingine. Unahitaji muda mwingi wa vitendo na mazoezi, lakini vyuo vingi havina mazingira bora ya mafunzo hayo,” anaeleza.
Anashauri Serikali kuifanya Lugha ya Alama ya Tanzania kuwa somo la lazima kuanzia shule ya msingi hadi vyuo vikuu, akisisitiza… “sisi sote ni viziwi watarajiwa, hivyo tunapaswa kujiandaa mapema.”
Kwa upande wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM), mhadhiri msaidizi Jafar Salum anasema wamekuwa wakifundisha Lugha ya Alama kwenye Shahada ya Sanaa ya Mawasiliano ya Umma kwa wanafunzi wa mwaka wa pili.
“Kwa wanafunzi wetu wa simesta ya kwanza na ya pili, somo la Lugha ya Alama ni la lazima kwa lengo la kuwapunguzia changamoto za mawasiliano wanapokutana na jamii ya viziwi na wawe na uwezo wa kutoa taarifa zao kwa usahihi kwenye jamii” anasema.
Hata hivyo, anabainisha kuwa kwa upande wa walimu somo hili ni la hiari, jambo linaloonesha bado halijapewa hadhi ya kitaifa.
Joseph Degera, mdau wa lugha ya alama kutoka Dodoma, anasema licha ya ongezeko la vyuo vinavyofundisha elimu maalum kama Mpwapwa, Dodoma na Kabaka, kuna upungufu mkubwa wa walimu wanaobobea katika lugha ya alama.
“Bado somo hili halijapewa uzito kama Kiswahili na Kiingereza. Hata Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) limechelewa kuandaa mwongozo rasmi wa wakalimani wa lugha ya alama,” anasema.
Degera anaongeza kuwa upungufu wa walimu na wakalimani wenye ujuzi unaathiri huduma muhimu kama afya na elimu.
“Fikiria mgonjwa kiziwi akifika hospitali bila mkalimani. Anawezaje kueleza tatizo lake kwa siri kati yake na daktari?” anauliza kwa taharuki.
Anashauri Lugha ya Alama iwekwe rasmi katika mitalaa ya elimu na kufundishwa kama lugha nyingine za kigeni, ili Watanzania wote waweze kuijua na kuitumia.
Walimu shuleni safari ni ndefu
Kwa upande wa shule za msingi na sekondari, changamoto zinabaki kuwa zilezile, uhaba wa walimu, ukosefu wa vitabu, na mtalaa usiotekelezwa ipasavyo.
Mwalimu Karim Bakari wa shule ya msingi Buguruni Viziwi, anasema walimu wachache waliopewa mafunzo maalum wamepewa majukumu mengine, na wengi hawapati mafunzo ya kuendeleza ujuzi wao.
“Walimu wengi hujifunza kwa kujitolea, kupitia semina za mara chache au hata wanafunzi wao. Serikali haijawahi kutoa mafunzo maalum ya lugha ya alama kwa walimu wa kawaida,” anafafanua.
Mwalimu huyo ambaye naye hasikii anaeleza kuwa matokeo ya wanafunzi wasiosikia katika shule za msingi si mabaya, lakini hali ni tofauti kwenye shule za sekondari kutokana na changamoto za mawasiliano na uhaba wa walimu.
“Serikali ianzishe idara maalum ya kuratibu lugha ya alama na kuhakikisha somo hili linafundishwa hadi vyuo vikuu,” anashauri.
Naye Mako Abubakar, mwalimu wa lugha ya alama, anasema walimu wengi wanafundisha bila vifaa vya kuona kama vitabu vyenye picha, michoro au video zinazoelezea alama kwa vitendo.
“Mfano, ukimwambia mtoto ‘baba anakwenda shambani’ na ukaonyesha picha ya mtu akibeba jembe, anaelewa kwa haraka zaidi. Lakini vifaa kama hivyo havipo, jambo linalowafanya wajifunze kwa ugumu,” anasema.
Kwa upande mwingine, walimu wa shule ya msingi Temeke, wakiongozwa na Heri Ngalisoni na Christopher Mgaya, wanasema changamoto nyingine ni wanafunzi kuzoea alama za nyumbani ambazo hutofautiana na zile rasmi za kitaifa.
“Tunaiomba jamii kushirikiana nasi. Mtoto akirudi nyumbani, azungumze kwa alama na nduguze ili apate mazoezi. Hilo litasaidia sana,” anasema Mgaya, akibainisha kuwa mwaka 2023 wanafunzi saba wa shule hiyo walifaulu wote kujiunga na sekondari.
Ofisa Elimu Maalum wa Jiji la Dar es Salaam, Saleh Msechu, anasema Serikali tayari imeandaa muongozo rasmi wa Lugha ya Alama ya Tanzania unaotumika nchi nzima.
“Zamani kila mkoa ulikuwa na alama zake, lakini sasa kuna mwongozo mmoja. Wizara imeandaa kamusi ya Lugha ya Alama, CD na miongozo ambayo imesambazwa nchini kote,” anasema.
Msechu anabainisha kuwa katika mtalaa mpya, lugha ya alama ni somo la lazima kwa walimu wote wanaosomea ualimu wa msingi na sekondari.
“Vyuo vyote vya ualimu vinapaswa kufundisha lugha ya alama kwa sababu elimu jumuishi sasa ni kipaumbele cha Taifa. Hata walimu walioko kazini wanapatiwa mafunzo mafupi kupitia halmashauri zao,” anasema.
Anasema Serikali pia inaendelea kuongeza walimu wa elimu maalum, huku vyuo kama Patandi vikipewa jukumu la kuzalisha wataalamu hao.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya walemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Jonas Lubago anasema kwa umuhimu wake, anaiomba serikali kuifanya lugha ya alama ya Tanzania kuwa lugha rasmi ya tatu ya kufundishia ngazi zote za elimu hapa nchini.
“Kama tumekubaliana Kiswahili kiwe lugha ya taifa na Kiingereza lugha rasmi, sisi tunaomba lugha ya alama iongezwe na kuwa rasmi katika matumizi hapa nchini”, anasema Lubago alipozungumza na Mwananchi.
Aidha ameomba wasahihishaji wa mitihani ya viziwi wajengewe uelewa ili kuwatendea haki wanafunzi hao ambao kwa kawaida sarufi na muundo wa sentensi kwa lugha ya alama ni tofauti na lugha nyingine.