Dar es Salaam. Wakati Lucy John (si jina lake halisi) alipohitaji msaada wa kifedha kwa dharura, aliamua kukopa taasisi moja ya fedha ya mikopo midogo (jina limehifadhiwa).
Taasisi hiyo ilikubali ombi lake haraka na kumpatia mkopo wa Sh20 milioni, jambo lililompa faraja.
Hata hivyo, hakusoma kwa makini masharti ya mkopo huo, kitu pekee alichokumbuka ni kuwa, riba ilikuwa asilimia 20.
Baada ya miezi mitatu, Lucy alipata funzo gumu la kutosoma masharti madogo ya mkataba. Alipochelewa kulipa kwa miezi mitatu, alilipa Sh15 milioni, lakini aliambiwa bado anadaiwa Sh5 milioni za mtaji, Sh12 milioni za adhabu na Sh12 milioni nyingine za riba.
“Nilishtuka sana. Ingawa nilijua riba ni Sh4 milioni, sikutarajia adhabu kubwa hivyo. Nilijaribu kujadiliana na ofisa mkopo ili wapunguze adhabu, kwa sababu nilipanga kumaliza deni Desemba, lakini alisisitiza lazima nilipie kiasi chote cha fedha,” amesema Lucy.
Kisa cha Lucy ni somo muhimu kwa wote wenye nia ya kukopa, wanapaswa kusoma na kuelewa masharti ya mikataba yao ya mikopo kabla ya kuisaini.
Inaelezwa asilimia kubwa ya watu wanaoomba mikopo nchini hujikuta wakisaini mikataba yenye gharama kubwa kwa sababu ya kupuuza mambo muhimu kama ya kiwango cha riba, muda wa marejesho na adhabu za ucheleweshaji wa marejesho.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mara kwa mara imeonya wananchi dhidi ya kukopa kutoka taasisi za kifedha zisizo na leseni, zikibainisha kuwa, taasisi hizo huwanyonya wakopaji kwa kutoza riba kubwa kupita kiasi, ada zilizofichwa, na adhabu kali.
BoT imeeleza kuwa, baadhi ya wakopeshaji wamekuwa wakitoza hadi asilimia 20 ya riba kwa mwezi.
Ili kuwalinda watumiaji wa huduma hizo, BoT imeanzisha Mwongozo wa Ada na Tozo kwa Watoa Huduma za Mikopo Midogo wa mwaka 2024, unaowataka wakopeshaji walio na leseni kuonyesha wazi viwango vyao vya riba, ada na adhabu kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza. Pia, lazima wapate kibali cha BoT kabla ya kuongeza au kubadilisha tozo hizo. Mwongozo huo umepiga marufuku ada za uendeshaji kama gharama za usimamizi au uchunguzi ili kuepuka mzigo usio wa haki kwa wakopaji.
Taasisi zitakazokaidi masharti hayo zinaweza kutozwa faini ya hadi Sh20 milioni 20 na hata kusitishiwa au kufutiwa leseni.
Aidha, BoT imewahimiza wananchi kuthibitisha iwapo taasisi wanayokusudia kukopa ina leseni, kwa sababu kuendesha biashara ya mikopo bila leseni ni kosa la jinai chini ya Sheria ya Mikopo Midogo ya mwaka 2018.
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba akizungumza na gazeti dada la The Citizen hivi karibuni kuhusiana na hoja hiyo, amesisitiza umuhimu wa kuelewa masharti ya mkopo kabla ya mtu hajaomba kupatiwa mkopa wa fedha.
“Wakopaji wanapaswa kutathmini uwezo wao wa kifedha na kuhakikisha wanaweza kulipa kwa wakati. Mkataba wa mkopo ni hati ya kisheria, kutojua masharti yake siyo sababu ya kujitetea,” amesema Tutuba.
Akizungumzia hilo, Katibu Mtendaji wa Chama cha Taasisi za Mikopo Midogo Tanzania (TAMFI), Winnie Terry, amesema wanachama waliopo chini ya chama hicho hawaruhusiwi kutoza zaidi ya asilimia 3.5 ya riba kwa mwezi.
“Sisi tunasimamia tu taasisi zilizo chini ya chama chetu. Wale wanaofanya kazi nje ya mfumo huu hawako chini ya uangalizi, ndiyo maana BoT imeelekeza watoa huduma wote wa mikopo midogo wasajiliwe,” amesema.
Ameongeza kuwa viwango vya adhabu hutofautiana kati ya taasisi, jambo linalowalazimu wakopaji kusoma kila kipengele cha mkataba kwa makini.
Mchambuzi wa masuala ya kifedha, Christopher Makombe amesema baadhi ya taasisi za mikopo midogo bado zinatoza riba haramu hadi asilimia 20 kwa mwezi, sawa na zaidi ya asilimia 790 kwa mwaka, hali inayowafanya wakopaji kubaki katika mzunguko wa madeni.
“Viwango hivi ni vya unyonyaji, vinakwamisha ukuaji wa kaya na biashara ndogo ndogo na kuvuruga uthabiti wa kifedha wa familia,” amesema.
Makombe ameiomba BoT na Tume ya Ushindani wa Haki (FCC), kuimarisha uangalizi, kuweka kikomo cha riba na kuhakikisha uwazi katika mikataba ya mikopo. Pia, amesisitiza haja ya kuongeza elimu ya fedha kwa wananchi.
“Wakopaji wengi husoma mikataba bila kuelewa riba ya mchanganyiko, adhabu au athari za kuchelewa kulipa,” amesema Makombe.
Ametoa rai kwa wakopaji wa fedha wote kusoma kwa makini masharti yote, waulize maswali na wahakikishe mkopo unaendana na uwezo wao wa kurejesha.