Mbeya. Mgombea urais wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Kyara amesema akipewa ridhaa ya kuongoza nchi ataweka mkazo katika kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa ili kusaidia wanaume kuondokana na woga na wakati huohuo kuwekeza katika tafiti za mimea tiba.
Akizungumza leo Jumanne, Oktoba 21, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika stendi ya mabasi mji mdogo wa Mbalizi, mkoani Mbeya, Kyara amesema familia haiwezi kuendelea bila mchango wa mwanamume, na akabainisha kuwa kauli hiyo haimaanishi kuwadharau wanawake, bali anapendekeza kuwezeshwa kiuchumi kwa sababu wana uwezo mkubwa wa kujitegemea.
“Familia yoyote bila mwanamume haiendi. Hii si kusema nawadhalilisha au kuwasahau wanawake, bali wao wataendelea kupewa nguvu kiuchumi kwa sababu wanaweza,” alisema Kyara.
Ameongeza kuwa, ili taifa liweze kusonga mbele kwa umoja, ni muhimu kuwepo kwa usawa wa kijinsia wa kweli.
Ameonya kuwa endapo hatua hazitachukuliwa, ipo hatari ya kujenga jamii yenye wanaume waoga na wanawake jasiri, jambo alilosema si afya kwa ustawi wa taifa.
“Tumepambana sana na changamoto za usawa wa kijinsia. Ni muhimu sana tukaliangalia suala hili kwa makini. Kupitia katiba ya SAU, tumelipa kipaumbele ili kila kundi katika jamii liwe na nafasi sawa,” amesema Kyara.
Aidha, mgombea huyo ameahidi kuwa serikali yake itawekeza zaidi katika tafiti za mimea tiba ili kusaidia wananchi kupambana na magonjwa sugu, ikiwemo saratani na Ukimwi, na kuchochea uchumi kupitia uvumbuzi wa dawa asilia.

“Tukifanya tafiti tukapata dawa za magonjwa kama Kansa na Ukimwi, watu kutoka mataifa mengine watakuja kununua hapa nchini. Hii itachochea ukuaji wa uchumi na kupunguza tatizo la ajira,” ameongeza Kyara.
Akizungumzia tatizo la ukosefu wa ajira, Kyara amesema chama chake kimeweka vipaumbele vitatu katika ilani ya uchaguzi ambavyo ni kilimo, viwanda na teknolojia, akisisitiza kuwa utekelezaji wa maeneo hayo utasaidia kufungua fursa nyingi za ajira kwa vijana.
Pia ameahidi kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa kujenga mabwawa makubwa 70 ya kuhifadhi maji ya mvua kwa ajili ya umwagiliaji, hatua itakayosaidia kuendeleza kilimo cha kisasa na kuongeza uzalishaji.
“Tumejaaliwa vyanzo vingi vya maji lakini hatuna miundombinu ya kuvihifadhi. Serikali ya SAU itajenga mabwawa makubwa ya kuvuna maji ya mvua kwa matumizi ya kilimo cha umwagiliaji,” alisema Kyara.
Kwa upande wake, Esau Nkusa mkazi wa Mbalizi aliyehudhuria mkutano huo, alisema wananchi wa eneo hilo wanahitaji viongozi watakaotoa suluhisho kwa changamoto za ajira, barabara na huduma za maji.
“Vijana wasomi ni wengi mitaani bila ajira. Miundombinu ya barabara ni mibovu na maji ni tatizo. Tunataka viongozi watakaoshinda wachukue hatua,” amesema Nkusa.