LUTANDULA KULA SAHANI MOJA NA MAWINGA PEMBEJEO

Kulia ni mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Chato kusini, Paschal Lutandula akiwa na mgombea udiwani kata ya Iparamasa (Kushoto) Peter Mbasa.

………………

CHATO 

KATIKA kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo cha kisasa ikiwa ni pamoja na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato kusini, Paschal Lutandula, ameahidi kula sahani moja na mawakala feki wanaopandisha ovyo pembejeo za kilimo.

Hatua hiyo inayotokana na ukosefu wa pembejeo za kilimo kwa wakulima wa kata ya Iparamasa wilayani Chato mkoani Geita, ambao baadhi yao wamekuwa wakiuziwa kwa bei kubwa licha ya pembejeo hizo kuwa na ruzuku ya serikali.

Lutandula amesema hayo akiwa kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Kijiji cha Songambele kata ya Iparamasa wilayani humo, wakati akiendelea kuomba kura kwa ajili ya kuwachagua wagombea wa Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Hayo yanajili huku zikiwa zimesalia siku nane kufanyika kwa Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani utakao fanyika Oktoba 29 mwaka huu.

“Ninataka kilimo kimnufaishe mkulima, mkinichagua kuwa Mbunge wenu nitaingia Bungeni kuhakikisha pembejeo zenye ruzuku ya serikali zinawafikia hadi wakulima wa bustani waliopo hapa Songambele”,

“Nitakwenda kusimamia kilimo na maslahi ya wakulima wote wa Jimbo letu, nitahakikisha mbegu bora zinakuja, mbolea na sumu za kuulia wadudu ili kila mkulima anufaike na kilimo chake” amesema Lutandula.

Vile vile amesema changamoto ya barabara ya kutoka Kijiji cha Songambele kwenda Nyarusunguti hadi Runzewe anaitengeneza ili kuwarahisishia wananchi wa kijiji hicho kwa lengo la kusogeza karibu maendeleo ya wananchi.

“Naomba wananchi muamini kuwa mimi nataka kuwa Mbunge wa maendeleo ya wananchi, nitakuwa mtumishi wenu kweli kweli, mkinichagua nitawalipa maendeleo” amesema Lutandula.

Diwani wa kata ya Iparamasa, Peter Mbasa, ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi kwa kumuamini kuwa diwani wao kwa miaka mitano iliyopita huku akiahidi kukamilisha baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo haikutekelezwa kwa kipindi kilichopita.

Kadhalika amemuomba mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato kusini kushughulika na changamoto ya askari wa hifadhi ya Runzewe, ambao wamekuwa wakiwabambikiza wananchi makosa ya kufanya biashara ya bangi pamoja na uuaji wa wanyama poli kinyume cha sheria, iwapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo.

                             Mwisho.