Mbeya ‘Derby’ ndani ya KMC Complex

KWA mara ya kwanza katika historia, mechi ya Watani wa Jadi wa Jiji la Mbeya, Mbeya Derby baina ya Mbeya City na Tanzania Prisons inachezwa Dar es Salaam na leo timu hizo zitakutana kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.

Mechi hiyo inalazimika kuchezwa hapo kutokana na Uwanja wa Sokoine uliopo Mbeya ambao huwa unatumika mara kwa mara kwa mechi hiyo kufungiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na kutokidhi vigezo vya kutumika kwa mechi za Ligi Kuu na Ligi ya Championship.

Wenyeji Mbeya City inaingia katika mechi ya leo ikiwa imetoka kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 kwenye mechi iliyopita ikiwa ugenini uwanjani hapo dhidi ya KMC.

MBE 01

Ushindi huo uliifanya Mbeya City ipande kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikifikisha pointi saba ambazo imekusanya katika mechi nne.

Tanzania Prisons nayo ilitoka kupata ushindi katika mechi ya mwisho ya Ligi iliyocheza na KMC kwa bao 1-0 lakini kabla ya hapo ilikuwa imepoteza mechi mbili za mwanzo dhidi ya Namungo na Tanzania Prisons ikifungwa bao 1-0 katika kila mechi jambo lililoifanya iwe nafasi ya 13 kwenye msimamo ikiwa na pointi tatu.

Akizungumzia mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Mbeya City, Malale Hamsini amesema: “Tumejiandaa kupata matokeo dhidi ya Prisons kesho (leo), huku tukijua kabisa tunakwenda kukutana na moja ya timu nzuri.”

Kiungo wa Tanzania Prisons, Masoud Abdallah ‘Cabaye’ amesema wamejiandaa vizuri kwa mechi hiyo.

MBE 02

“Hatuko katika nafasi nzuri hivyo tunahitajika kupata ushindi ili tusogee juu. Maandalizi tuliyofanya ni mazuri,” amesema Cabaye.

Rekodi zinaonyesha Tanzania Prisons imeshinda mechi sita za dabi hiyo, huku Mbeya City ikiibuka na ushindi mara tano. Sare ni tisa katkka mechi 20 tangu msimu wa 2013-2014.

Mara ya kwanza zilikutana Oktoba 29, 2013, Mbeya City ikiwa mgeni iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, huku Tanzania Prisons ikilipa kisasi mara ya mwisho kukutana iliposhinda 2-1, Desemba 25, 2022 ambapo Mbeya City ilikuwa mwenyeji wa mechi hiyo.