Mgombea udiwani Kirua Vunjo Magharibi afariki dunia

Moshi. Mgombea udiwani wa Kata ya Kirua Vunjo Magharibi, Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), John Kessy amefariki dunia leo, Oktoba 21, 2025.

Akizungumza na Mwananchi, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Mahanyu amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kueleza kuwa amefariki dunia leo saa nane mchana katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi mjini Moshi.

“Ni kweli tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mgombea wetu, Ndugu John Kessy, kilichotokea leo saa nane mchana akiwa hospitali ya Mawenzi,” amesema Mahanyu.

Hata hivyo, taarifa za chanzo cha kifo cha mgombea huyo bado hazijatolewa rasmi na viongozi wa chama hicho.

Kifo cha mgombea huyo kimetokea ikiwa zimepita siku chache tangu kutokea kifo cha mgombea ubunge kupitia chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Siha, Daudi Ntuyehabi (34), aliyefariki dunia Oktoba 7, mwaka huu.