Mgombea udiwani Pasua aahidi kuwakwamua vijana kiuchumi

Moshi. Mgombea udiwani wa Kata ya Pasua, Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Barreh Farrah, ameahidi kuwa endapo atapewa ridhaa ya kuongoza kata hiyo, atahakikisha anawaunganisha vijana wasio na ajira na taasisi binafsi ili kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo Jumanne, Oktoba 21, 2025, katika eneo la mwisho wa daladala za Pasua, Farrah alisema mpango huo unalenga kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wa kata hiyo.

“Nitahakikisha ninatekeleza vyema Ilani ya CCM kwa kutumia mahusiano mazuri niliyojenga na viongozi wa serikali, chama, na wakurugenzi wa makampuni mbalimbali,” alisema Farrah.

Amesema atatumia uhusiano huo kuwaunganisha vijana na taasisi binafsi zinazotoa ajira au fursa za kujiajiri, ili waweze kujipatia kipato na kukuza maendeleo ya kiuchumi.

“Nitatumia nafasi hii kusaidia vijana kupata ajira kwa makundi na hata mtu mmoja mmoja, ili waweze kujikwamua kibiashara na kimaendeleo,” ameongeza.

Kuhusu miundombinu, mgombea huyo ameahidi kufanikisha ujenzi wa barabara inayoanzia mwisho wa daladala za Pasua hadi soko la Relini (Texas) kwa kiwango cha lami, pamoja na ufungaji wa taa za barabarani ili kuboresha usalama na mandhari ya eneo hilo.

Mgombea ubunge wa Viti Maalum kupitia Jumuiya ya Wazazi Taifa (CCM), Dk Catherine Joachim akizungumza na wananchi wa kata ya Pasua kwenye mkutano wa kampeni ambao umefanyika katika eneo la mwisho wa daladala za Pasua, mjini Moshi.Picha na Janeth Joseph

“Maono yangu ni kuona barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami na kuwekwa taa za barabarani. Naomba mnichague Oktoba 29 ili nisimamie utekelezaji wake,” amesema Farrah.

Kuhusu mikopo ya Halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Farrah aliahidi kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa kwa wakati na zinatumika kwa tija.

“Nitaleta wataalamu kuwafundisha namna bora ya kutumia mikopo hiyo ili iweze kuwainua kiuchumi,” amesema.

Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Viti Maalum kupitia Jumuiya ya Wazazi Taifa (CCM), Dk Catherine Joachim, amewataka wananchi wa Pasua kuwachagua wagombea wa CCM katika nafasi zote, akiwemo mgombea urais, Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa ameongoza nchi kwa mafanikio makubwa.

“Kupitia filamu ya The Royal Tour, watalii wameongezeka nchini, jambo lililowezesha vijana kupata ajira katika sekta ya utalii na wananchi wengi kunufaika kwa kuuza bidhaa mbalimbali katika mazingira ya amani,” amesema Dk Catherine.

Aidha, amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia imefanya maboresho makubwa katika sekta ya afya mkoani Kilimanjaro, ikiwemo kuboresha Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi na KCMC, hali iliyowezesha wananchi kupata huduma bora zaidi za afya.

Dk Catherine pia amewataka wananchi wa Pasua kumchagua mgombea ubunge wa CCM wa Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, akisema ni kiongozi mwenye uwezo wa kuwaunganisha wananchi na kusukuma maendeleo ya kweli katika jimbo hilo.