:::::::::::
Na Mwandishi Wetu
Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza kuwa mitihani ya upimaji wa kitaifa kwa darasa la nne inaanza rasmi kesho, Oktoba 22, 2025, kote nchini.
Kwa mara ya kwanza, upimaji huu utafanyika kwa mujibu wa mtaala mpya unaozingatia Sera ya Elimu ya mwaka 2014 toleo la 2023. Lengo kuu la mtaala huu ni kupima uelewa wa kina wa wanafunzi katika stadi za kusoma, kuandika, kuhesabu na maarifa ya kijamii.
Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, amesema jumla ya wanafunzi milioni 1.58 wamesajiliwa kufanya mtihani huo, ambapo wavulana ni 768,290 sawa na asilimia 48.31 na wasichana ni 817,850 sawa na asilimia 51.69.
Wanafunzi hao watafanya mitihani ya masomo sita ya msingi, ikiwemo Sayansi yenye Hisabati, Jiografia na Mazingira. Kwa upande wa sanaa, watafanya Kiswahili, Kiingereza, Historia ya Tanzania na Michezo.
Aidha, kutakuwa na masomo ya uchaguzi ambapo wanafunzi wataweza kuchagua lugha mojawapo kati ya Kichina, Kiarabu au Kifaransa kama somo la ziada.
Profesa Mohamed amesema takribani wanafunzi 106,503 watafanya upimaji wa lugha ya Kiingereza, sawa na asilimia 6.7, huku waliopanga kufanya Kiswahili wakifikia milioni 1.475.
Katika kundi hilo, wanafunzi wenye mahitaji maalumu ni 5,750, wakiwemo 1,164 wenye uoni hafifu, 111 wasioona, 1,161 wenye uziwi, 1,641 wenye ulemavu wa akili, na 1,673 wenye ulemavu wa viungo.
Upimaji huu utafanyika kwa siku mbili, Oktoba 22 na 23, na masomo sita ya msingi yamechaguliwa kwa umakini na wataalamu waliobobea ili kuhakikisha tathmini inakuwa sahihi na ya haki kwa kila mwanafunzi.