Njombe. Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amewataka wananchi kutumia fursa iliyopo ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya zao na mazingira yanayowazunguka, kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Mkoa wa Njombe umezindua rasmi mradi wa usambazaji na uuzaji wa majiko bunifu kwa bei ya ruzuku ili kuhakikisha wananchi wote wanatumia nishati safi.
Uzinduzi wa mradi huo umefanyika leo Oktoba 21,2025, na Mkuu wa wilaya ya Ludewa, OlivanusThomas kwa niaba ya Mtaka uliofanyika wilayani Ludewa mkoani Njombe.
Amesema lengo la mradi huo ni kuutambulisha rasmi mradi wa matumizi bora ya nishati kwa wananchi wa mkoa huo ambao ndiyo walengwa na wanufaika wakubwa.
Amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yamelenga kutunza afya kwa watumiaji lakini pia kuhifadhi mazingira na kuondoa ukataji wa miti ovyo kwa ajili ya kutafuta kuni na mkaa.
Amepongeza juhudi za Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo ambapo amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha mkakati wa nishati safi ya kupikia ni kuwa kufikia 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanaitumia.
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Olivanus Thomas katikati akiwa katika uzinduzi wa wa usambazaji na uuzaji wa majiko bunifu yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi mkoani Njombe
“Serikali imeweka ruzuku ya asilimia 85 kwa hiyo kina baba na kina mama wa Mkoa wa Njombe wajiandae kutumia majiko banifu kwani mradi huu kwetu ni neema” amesema Thomas.
Mhandisi wa miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), David Malima amesema mradi huo umekuja kwa ajili ya kuimarisha na kuboresha afya za wananchi ,mazingira ,kukuza upatikanaji wa nishati safi na endelevu.
Amesema lengo lingine ni kupanua usambazaji wa nishati mbadala katika maeneo ya vijijini na zaidi kuhamasisha matumizi ya teknolojia safi na bora za kisasa ya kupikia.
“Mradi huu unatarajia kugharimu zaidi Sh285.3 milioni kwa Mkoa wa Njombe pekee na utafanikisha uuzaji na usambazaji wa majiko banifu 4,836,” amesema Malima.
Amesema uuzaji na usambazaji wa majiko banifu utafanyika katika wilaya nne (4) ambazo ni Wilaya ya Njombe, Ludewa, Wanging’ombe na Makete ambapo kila wilaya majiko banifu 1,209 yatasambazwa na kuuzwa kwa bei ya ruzuku.
Mkazi wa wilaya ya Ludewa Ariph Gwivaha amesema: “Ujio wa mradi huu ni mkombozi kwetu utatusaidia kutunza afya zetu kwani matumizi ya kuni na mkaa yalikuwa yanatuathiri sana.”