Mtoto wa aliyekuwa Rais wa pili Zanzibar afariki dunia, kuzikwa leo

Unguja. Mussa Aboud Jumbe mtoto wa aliyekuwa Rais wa pili wa Serikali ya Mapainduzi ya Zanzibar (SMZ), Aboud Jumbe amefariki dunia wakati akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar.

Mussa ambaye alikuwa mtoto wa mwisho, amefariki usiku wa kuamkia leo Oktoba 2021 katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kutokana na tatizo la kupumua.

Kaka wa marehemu, Dk Aboud Jumbe amethibitisha kifo hicho na kusema maziko yanatarajiwa kufanyika leo Oktoba 21, 2025 saa 10:00 jioni katika makaburi ya familia Migombani Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akizungumza na Mwananchi, mtoto wa kaka yake Slayyum Mustapha Aboud Jumbe amesema marehemu ameugua kwa muda mrefu, alipelekwa nchini India kwa matibabu kisha kurejeshwa nchini.

Amesema siku ya Jumamosi (Oktoba 18, 2025), hali yake ilibadilika kutokana na kupata shida ya kupumua ndipo alipelekwa katika hospitali ya Mnazimmoja na kulazwa katika chumba cha maututi ambapo umauti umemkuta.

“Marehemu aliumwa kwa muda mrefu, alipelekwa India na kisha akarejeshwa kwa hiyo alilazwa hospitali ya Mnazi mmoja na umauti umemkuta hapo,” amesema.

Amesema kabla ya kifo chake marehemu aliagiza akifa azikwe nyumbani kwao alipozikwa baba yake kwa hiyo swala na maziko vitafanyika hapo Migombani. “Kwa sasa tupo kwenye vikao vya familia kuandaa mazishi na maziko,”  amesema.