Dodoma. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu amesema hatapenda kuona vumbi katika Jiji la Dodoma pindi atakapokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwalimu ametoa ahadi hiyo leo Jumanne Oktoba 21, 2025 katika kampeni za kunadi ilani ya chama hicho ili apate ridhaa ya kuiongoza nchi.
Mkutano huo wa kampeni umefanyika katika Kijiji cha Ngh’ambaku kilichopo Wilaya ya Chamwino, jijini Dodoma.
Amegusia suala hilo alipokuwa akijibu namna watakavyoshughulikia changamoto za barabara zinazolikabili Jimbo la Mvumi zilizoelezwa na mgombea ubunge kupitia Chaumma, Mwanga Chibago.
Katika maelezo yake, amesema changamoto hiyo hataitatua tu kwa Mvumi, bali Dodoma nzima na anataka kulifanya jiji hilo wageni wakifika, waone heshima ya Taifa kupitia sura ya makao makuu ya nchi.

Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu
“Sitashughulikia barabara za Mvumi tu, bali ninataka kuijenga Dodoma katika kiwango ambacho dunia huwa inajenga makao makuu yao na kuondoa barabara zote zinazoitwa za vumbi, kwa kuwa uwezo huo tunao, ni watu tu wameshindwa kuamua,” amesema Mwalimu.
Pia, amesema watu wa Mvumi hawakupaswa kulia na kero ya barabara kwa kuwa ni sehemu inayozalisha zao la zabibu linalobeba uchumi wa jiji hilo.
“Nendeni nchi ya Afrika Kusini wanalima zabibu na ukienda mashambani kwao unakutana na lami zilizonyooka kwa kuwa ndio uchumi wao,” amesema.
Mgombea huyo, pia, amegusia suala la mgogoro wa mipaka ya Hifadhi ya Ruaha na makazi ya wananchi na kueleza kuwa, hakukuwa na sababu ya ardhi yao kumegwa kwa kisingizio cha idadi ya wanyama kuongezeka.
“Suala la kuongezwa hifadhi ya Ruaha, sababu eti swala wameongezeka, tembo, digidigi, kwani ninyi hamuongezeki, mnaenda kujenga wapi kama eneo linagawiwa kwa wanyama na hapa mlipo bado mnahitaji ardhi ya kilimo ya mifugo,” amesema Mwalimu.
Amesema jambo hilo la ardhi ni kielelezo tosha kuwa kama bado kuna mtu anakiunga mkono chama kilichopo madarakani, hataiona pepo.
“Kwani Mungu si aliwaumba mzaliane, yaani Mungu anasema nendeni mkaijaze dunia halafu wanawanyima ardhi, wawapelekeni basi mbinguni, maana kuna ardhi na mbingu sasa si wamewanyima ardhi,” amesema.
Katika ahadi yake upande wa ardhi, amesema msimamo wake akiingia madarakani, ni kwenda kuirudisha ardhi iliyochukuliwa kinyemela kwa wananchi sababu changamoto kama hizo amezikuta Kilosa na Serengeti.

Kuhusu barabara , Mwalimu amesema wakazi wa Mvumi wanalipa Sh10,000 ya nauli kwa sababu mwenye gari anafidia kulipa uchakavu wa gari lake kunakochangiwa na ubovu wa barabara, sehemu ambayo kihalali wangepaswa kulipa Sh1,500 hadi Sh2,000.
“Kama basi linatoka Dar kwenda Moro kilometa 200 ni Sh13,000 kwanini huku nauli iwe Sh10,000 na kuna kideo, unapata biskuti na soda juu.
“Lakini huku kwenu mnapanda na baiskeli hukohuko, kuku, mbuzi na mnalipa hela yote hiyo, fikiria hiyo Sh8,000 iliyozidi ungefanya mambo mangapi ya maendeleo,”amesema
Kuhusu afya, mgombea huyo ameshangaa mji kama Mvumi unakosa kituo cha afya na kueleza kwamba, hayo ni matokeo ya kuwang’ang’ania viongozi walewale miaka nenda rudi na kutaka wafanye mabadiliko kuweka viongozi wenye nia njema nao.
“Niwaulize tu mnaenda kujifungulia wapi kinamama wa hapa, lakini pia niwaulize hapa madiwani walioko hapa ni chama gani, mbunge ni wa chama gani na kura nyingi si mlipeleka kwa Rais nyie, haya kiko wapi sasa?” amehoji Mwalimu.
Mgombea ubunge Jimbo la Mvumi, Mwanga Chibago amesema kata waliyofanyia mkutano ni moja kati ya 22 zilizopo katika jimbo hilo na alichagua kwa makusudi ili mgombea urais ashuhudie changamoto walizonazo wananchi ili akichaguliwa akazitatue.
Ukiacha barabara na masuala ya migogoro ya ardhi, mgombea ubunge huyo amesema kata hiyo haina shule ya sekondari, jambo linalowafanya wanafunzi kutembea kilometa sita kufuata shule na wengine kufikia hatua ya kukatiza masomo.
Wakati kwenye afya amesema kunahitajika kituo cha afya, kila kata kuna tofauti ya kilometa 25 hadi 30 ambayo imekuwa ni changamoto kwa wananchi wa mvumi kupata haki ya afya.
Hata hivyo, mgombea ubunge huyo amemhakikishia mgombea urais huyo kuwa, kati ya jimbo atakalopata kura nyingi ni hilo la Mvumi kwa kuwa aliyepo ameshindwa kuleta heri kwa wakazi wa Mvumi.
Amesisitiza kuwa, atakuwa mbunge wa kwanza wa Chaumma kwenye Mkoa wa Dodoma na Jimbo la Mvumi.