Mirerani. Mgombea udiwani wa Kata ya Endiamtu, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Lucas Chimbason, amewaomba wakazi wa eneo hilo kumpa kura nyingi za ndiyo akisema anaiomba nafasi hiyo kwa nia ya kutumikia wananchi, si kutawala.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu wa kata ya Endiamtu uliofanyika Oktoba 21, 2025, katika viwanja vya Big Apple, Chimbason amesema wakazi wa Endiamtu ni watu waungwana na kwamba endapo watampa ridhaa ya kuwa diwani wao, ataendelea kuwa mtumishi wao wa kweli.
“Ninaomba utumishi kwenu, si ubosi. Nimekuwa mtumishi wenu katika vipindi vya mwaka 2010–2015 na 2015–2020, mkani pumzisha kwa muda, lakini mwaka 2020–2025 mkaniamini tena. Mmeona jinsi nilivyojituma kuwatumikia,” amesema Chimbason.

Mgombea udiwani kupitia CCM kata ya Endiamtu wilayani Simanjiro mkoani Manyara Lucas Zacharia Chimbason (kushoto) akinadiwa na mmoja wa waliokuwa watia Issa Katuga kwenye mkutano wa kampeni ya kuomba kura kwa wakazi wa eneo hilo. Picha na Joseph Lyimo
Alieleza kuwa katika kipindi chake cha uongozi amesimamia miradi mingi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu na maji, na anaomba kipindi kingine ili kukamilisha miradi ya barabara iliyobaki.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na serikali ya awamu ya sita kwa kuipatia Endiamtu fedha za maendeleo. Pia tunawashukuru kampuni za Franone Mining kwa kujenga korido ya mochwari na Chusa Mining kwa kujenga wodi ya wanawake na watoto,” amesema.
Chimbason alitumia nafasi hiyo kuwaombea kura za ndiyo mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, na mgombea ubunge wa Simanjiro, James Ole Millya, akisema watakuwa chachu ya maendeleo katika ngazi ya taifa na jimbo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shule ya Glisten, Justin Nyari, amesema Chimbason ni kiongozi mzoefu na mwenye uchungu na maendeleo ya wananchi, hivyo anastahili kupewa nafasi nyingine ya kuendelea kuongoza.
“Kipindi cha mwaka 2010–2015 mimi nikiwa diwani wa Mirerani na Chimbason wa Endiamtu, tulianza udiwani kwa mara ya kwanza. Ni kiongozi mwenye moyo wa maendeleo, anastahili kuendelea,” amesema Nyari.
Naye Mgombea udiwani wa Kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer, amesema Chimbason ni kama pacha wake kisiasa, hivyo wananchi wa Endiamtu wampe kura nyingi za ndiyo.
“Kiongozi anayetumia fedha zake kusaidia maendeleo ya kata ni mtu wa kuungwa mkono, si wa kuachwa,” amesema Taiko.
Aidha, Issa Katuga, mmoja wa watia nia wa udiwani wa kata hiyo, alisema makundi ya kisiasa ndani ya CCM yameungana na kubaki kundi moja lenye lengo la kuhakikisha ushindi wa chama.
“Sasa hivi tupo kundi moja tu – CCM. Tumuunge mkono Chimbason kwa kura nyingi za ndiyo,” alisema Katuga.
Adam Kobelo, aliyewahi kuchuana na Chimbason katika mchakato wa kura za maoni, naye alimpongeza mgombea huyo akisema anatosha kuendelea kuiongoza Kata ya Endiamtu.
“Chimbason ni kiongozi makini na mchapakazi. Tunapaswa kumwunga mkono kwa kura nyingi ili aendelee na kazi nzuri aliyoianzisha,” amesema Kobelo.