Dodoma. Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma imeikubali rufaa iliyokatwa na Clinton Damas, maarufu Nyundo na wenzake waliotiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti kwa kundi, ikieleza kosa hilo halipo katika sheria.
Hata hivyo, mahakama hiyo imebariki kutiwa hatiani na adhabu ya kifungo cha maisha jela walichohukumiwa washtakiwa hao kwa kosa la kubaka kwa kundi, hivyo wataendelea kutumikia adhabu hiyo.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne, Oktoba 21, 2025 na Jaji wa Mahakama Kuu, Amir Mruma. Kwa kosa la kulawiti kwa kundi, amesema hakuna sheria kwa kosa hilo, bali adhabu hutolewa kwa mtu mmoja mmoja aliyetenda kosa hilo.
Mbali ya Nyundo, aliyekuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), warufani wengine ni aliyekuwa askari Magereza, Praygod Mushi, Nickson Jackson maarufu Machuche na Amin Lema ‘Kindamba’.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma iliwatia hatia na kuwahukumu kifungo cha maisha jela Nyundo na wenzake kwa mashtaka ya kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam, aliyetambulishwa mahakamani kwa jina la XY.
Hawakuridhika na kutiwa hatiani na hukumu hiyo, hivyo walikata rufaa Mahakama Kuu, wakiwakilishwa na mawakili Godfrey Wasonga, Roberth Owino na Meshack Ngamando, wakiwa na hoja 33 za rufaa walizoziweka kwenye mafungu tisa.
Miongoni mwa sababu za rufaa ni kukosewa kwa hati ya mashtaka, kutothibitisha kosa bila kuacha shaka na kushindwa kuwakamata watuhumiwa wengine wawili.