Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT- Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema akishinda urais Oktoba 29, ataviendeleza vipaji vya sanaa mbalimbali ili kutimiza malengo ya wasanii wa kisiwa hicho.
Othman amesema atahakikisha anaipa kipaumbele sekta ya sanaa kwa kuwajengea uwezo wasanii wa ndani kisiwa hicho, ili kufikia viwango vya kimataifa na kuitangaza Zanzibar duniani kupitia vipaji vyao.
Miongoni mwa vipaji ni pamoja na michezo ya sarakasi muziki, filamu na uchongaji, akiahidi kuisimamia vyema sekta ya sanaa kwa kuwekea miundombinu bora, maarifa na zana za kisasa.
“Mungu atujalie hii ndio kujenga nchi na Taifa,” amesema Othman leo Jumanne Oktoba 21,2025 akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Chambaa Jimbo la Chambani kisiwani Mkoa wa Kusini Pemba.
Katika maelezo yake, Othman amesema Zanzibar ina hazina kubwa ya wasanii kinachokosekana ni mazingira wezeshi ili kuwasaidia wasanii wa visiwani humo, lakini chini ya uongozi wake hatakuwa kikwazo kwa sekta hiyo kupiga hatua za maendeleo.

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman akizungumza na wananchi wa Jimbo la Chambani Mkao wa Kusini Pemba katika mwendelezo wa mikutano ya kampeni ya kusaka kura
“Serikali nitakayoiongoza itahakikisha sanaa inakuwa ajira rasmi na chanzo cha kipato. Tutaunda mfuko maalumu wa maendeleo ya sanaa, kukuza ubunifu na kutoa mafunzo ya kisasa kwa vijana wenye vipaji,” ameeleza.
Katika mkutano huo, Othman maarufu ‘OMO’ amesisitiza kuwa kipaumbele chake cha kwanza akishika madaraka ni wananchi atahakikisha Serikali atakayoiunda inawatumikia Wazanzibari si kuwatumikisha.
“Serikali yangu itawanyanyua na si kuwakanyaga wananchi, tutawaendeleza na si kuwadumaza. Muhimu mnipe funguo (kura yako) ili niingie Ikulu Oktoba 29,” amesema Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo.
Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Omar Ali Shehe amesema zimebaki siku chache kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika, akiwataka Wazanzibari kujitokeza Oktoba 29 ili kumpeleka Othman Ikulu.
“Jumamosi Mungu akijaalia tutafunga kazi kwa mkutano mkubwa utakaofanyika uwanja wa Tibirinzi, siku hiyo ACT Pemba tutakwenda kupiga kura Tibirinzi.
“Tumebakisha majimbo mawili kati ya 18 tuliopangiwa kwenda, kifupi tumemaliza kazi Oktoba 29, Othman anakwenda Ikulu,” amesema Shehe.