Dar es Salaam. Ili kuhakikisha ulinzi wa taarifa za mtumiaji, kuepuka udukuzi watumiaji wa simu janja (smartphones) na vifaa janja wanashauriwa kupakua programu tumizi, (Apps download) kutoka vyanzo rasmi ikiwemo Google Play Store’ na ‘Apple App Store’.
Kufanya hivyo kutaepusha udukuzi wa taarifa za mtumiaji kwakuwa programu hizo zimethibitishwa ikiwa ni tofauti na upakuaji kutoka vyanzo visivyo rasmi.
Ikumbukwe programu tumizi zinatumika kurahisisha shughuli mbalimbali ikiwemo mawasiliano, ununuzi wa bidhaa mtandaoni, usafirishaji, benki za kidijitali, hadi huduma mbalimbali za kijamii ambapo kila kitu kinafanyika kupitia simu janja au kompyuta.
Mara nyingi mtumiaji wa simu janja huweka akaunti yake binafsi yenye taarifa zake na wakati mwingine huweka taarifa ikiwemo za kibenki, pale anapopakuwa programu tumizi kwa zile zinazouzwa.
Hata hivyo, upo uwezekano wa kujitokeza kwa changamoto ya kiusalama kwenye mchakato wa kupakua baadhi ya programu hizo, pale mtumiaji atakaposhindwa kuzingatia hatua sahihi.
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kutopakua programu hizo katika vyanzo rasmi vinavyotambulika na vyenye uthibitisho wa usalama mfano wa ‘Google Play Store’ na ‘Apple App Store’.
Akizungumza na Mwananchi mtaalamu wa Tehama na mifumo yake, Dk Bakari Mashaka amesema: “Kwa mfano, kwenye simu janja za Android, programu salama huwa na alama ya ngao ya kijani (Play Protect), ilhali kwenye simu janja za iPhone huwa na baji maalum yenye rangi ya bluu au kijani”
“Vilevile, programu hizo zinapaswa kuwa na maelezo kamili kuhusu kampuni iliyozitengeneza, mawasiliano, tovuti rasmi, na sera ya faragha” amesema Dk Mashaka ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo cha Uhasibu Arusha kampasi ya Songea,” anasema.
Anasisitiza mtumiaji kuepuka programu zinazojitokeza kupitia matangazo unapotumia programu nyingine, kwa kuwa baadhi ya hizo si salama na zinaweza kudukua taarifa binafsi au za kifedha.
Anaeleza kuwa ili kujikinga na hatari hizo, tumia programu maalum za ulinzi dhidi ya programu hasidi (malware) zinazojulikana kama programu za kingavirusi (antivirus).
“Mifano ya programu hizo ni kama Google Play Protect, Avast, na nyinginezo zilizothibitishwa,” amesema.
Anaongeza kuwa ni muhimu kuhakikisha unasasisha (update) simu yako janja mara kwa mara ili kurekebisha mianya ya kiusalama inayoweza kutumiwa na wahalifu wa mtandaoni kuiba taarifa zako binafsi na kifedha.
Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya teknolojia, Anania Kapala anasema ni muhimu kabla ya kutumia programu tumizi kuhakikisha unasoma kwa umakini masharti pamoja na sera za faragha.
“Baadhi ya watu hupuuzia kusoma masharti (Terms and Conditions) au sera za faragha (Privacy Policy) kabla ya kukubali kutumia App, ni muhimu kuzisoma na kuzielewa kwani zinaeleza ni taarifa gani App inazichukua, inazitumiaje, na kama huzishirikisha na wadau wengine.
“Ni muhimu kuzisoma ili kuelewa haki zako na mipaka ya matumizi ya taarifa zako.”amesisitiza. Vilevile anasisitiza kutumia neno siri imara wakati wa kutumia programu hizo.
“Tumia mchanganyiko wa herufi kubwa, ndogo, namba, na alama maalumu, Epuka kutumia jina lako, tarehe ya kuzaliwa, au taarifa nyingine rahisi kubashiriwana usitumie nenosiri moja kwa akaunti nyingi,” amesema.
Anahimiza umakini wakati programu tumizi inahitaji kuchukuwa baadhi ya taarifa katika kifaa chako. Wakati mwingine App huomba ruhusa kama kamera, eneo ulipo, au orodha ya mawasiliano, Usikubali kila ruhusa bila kujua kwa nini inahitajika.
Given Edward ambaye ni mtaalamu wa masuala ya teknolojia anasema ni muhimu mtu kuhakikisha analinda barua pepe yake (email) kwa kuiwekea neno siri madhubuti. Kwani kupitia email mtu anaweza kupata taarifa nyingi za muhusika.
Pia, anahimiza matumizi ya Ulinzi wa Hatua Mbili (Two-Factor Authentication), kwani ni njia ya ziada ya usalama ambapo, hata kama mtu atapata nenosiri lako, hatoweza kuingia kwenye akaunti bila msimbo wa muda unaotumwa kwenye simu au baruapepe yako.
Vilevile anasisitiza kuepuka kugusa link zisizojulikana zimetokea wapi pamoja na matumizi ya ‘public wi-fi’ wakati wa kutumia akaunti zako za mi9tandao ya kijamii, benki au zinginezo rasmi.