Sababu watoto wengi wa kupandikiza kuzaliwa wa kiume

Dar es Salaam. Wazazi wengi huamini kuwa nafasi ya kupata mtoto wa kiume au wa kike ni sawa, yaani 50 kwa 50.

Lakini wale wanaopata watoto kupitia njia ya upandikizaji mimba kwa njia ya ‘In Vitro Fertilization’ (IVF) wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata mtoto wa kiume, kwa mujibu wa wanasayansi.

Utafiti mpya uliowasilishwa kwenye mkutano wa ‘New Scientist Live’ na kuripotiwa na gazeti Ia mtandaoni la Daily Mail la Uingereza la Oktoba 20, 2025 unaonyesha kuwa upendeleo wa kijinsia hutokea wakati wa uteuzi wa kijusi cha kupandikizwa.

Wataalamu wamebaini kwamba vijusi vya kiume hukua kwa kasi kidogo zaidi, na hivyo vina uwezekano mkubwa wa kuchaguliwa kwa ajili ya kupandikizwa tumboni.

Hali hii inaweza kueleza kwa nini nafasi ya kupata mtoto wa kiume kupitia IVF ni kubwa. Takwimu zilizotajwa kwenye utafiti huo zinaonyesha kwenye kila watoto 100 wanaozaliwa kwa njia hiyo, 56 ni wa kiume.

 “Unapohusianisha kasi kubwa ya ukuaji na ubora, kinachotokea ni kwamba unachagua kwa upendeleo vijusi vya kiume,” amesema Dk Helen O’Neill, mtaalamu wa masuala ya uzazi kutoka Chuo Kikuu cha London, “Vifaa tunavyovitumia vinaishia kuchagua zaidi vijusi vya kiume.”

Wakati vijusi vya kiume vina kromosomu moja ya X na moja ya Y, vile vya kike vina kromosomu mbili za X.

Moja kati ya kromosomu hizo za X huzimwa katika hatua za awali kabisa za ukuaji, hatua muhimu ya kusawazisha maumbile ya vinasaba, lakini inayohitaji nishati na rasilimali zaidi.

Kwa kuwa vijusi huchaguliwa kulingana na jinsi vinavyokua na kukomaa, vijusi vya kiume huwa na nafasi kubwa zaidi ya kuchaguliwa kwa sababu hukua kwa kasi kidogo zaidi katika siku chache za kwanza baada ya urutubishaji.

Utafiti wa awali ulibaini kwamba IVF husababisha uwezekano mkubwa zaidi wa kupata mtoto wa kiume, lakini wanasayansi hawakuwa na hakika kwa nini.

Dk O’Neill amesema maelezo yaliyokuwepo awali yalikuwa kwamba mazingira ya kukuza vijusi kwenye chombo cha maabara huenda yalifanya vile vya kiume kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuishi.

Lakini, utafiti mpya uliowasilishwa kwenye mkutano wa ‘New Scientist Live’ na kuripotiwa na mtandao wa ‘TheiPaper’ wa Uingereza na kunukuliwa kwenye Gazeti la Daily Mail, unaonyesha kuwa upendeleo wa kijinsia hutokea wakati wa uteuzi wa kijusi cha kupandikizwa.

Kihistoria, madaktari wamekuwa wakipima ubora wa vijusi kwa kuvitazama kupitia darubini.

Sasa, baadhi ya vituo vya uzazi vimeanza kutumia pia teknolojia ya akili bandia (AI) katika mchakato huo, kwa kutumia video za ‘timelapse’ zinazoonyesha jinsi kijusi kinavyokua hatua kwa hatua.

Timu ya Dk O’Neill ilifanya utafiti kubaini uwezekano wa kuchaguliwa kwa vijusi vya kiume au vya kike ama kwa madaktari au kwa mifumo miwili tofauti ya AI. Walichunguza vijusi 1,300 ambavyo jinsia yake ilijulikana kupitia vipimo vya vinasaba.

Matokeo yalionyesha kwamba wakati madaktari walipofanya uteuzi, walipanga asilimia 69 ya vijusi vya kiume kama vya ubora mzuri, ikilinganishwa na asilimia 57 ya vile vya kike.

Mfumo mmoja wa AI ulionyesha upendeleo mdogo kwa vijusi vya kiume, huku mwingine ukipima kwa usawa kati ya vya kiume na vya kike.

Katika mchakato wa IVF, mbegu za kiume huongezwa kwenye mayai kadhaa kwenye chombo maalumu kwa matumaini ya kutengeneza vijusi vingi iwezekanavyo.

Baada ya takriban siku tano, kijusi kinachoonekana kuwa na afya njema zaidi huchaguliwa kwa ajili ya kupandikizwa tumboni mwa mama.

Dk O’Neill alisema tofauti ya kasi ya ukuaji ni ndogo mno kiasi kwamba haiwezi kutumika kwa makusudi kuchagua mtoto wa kiume au wa kike.

Aidha, kuchagua jinsia ya mtoto kupitia IVF hairuhusiwi katika kliniki za Uingereza isipokuwa tu pale wazazi wanapokuwa na ugonjwa wa kurithi unaoathiri jinsia moja pekee.

Utafiti mwingine wa awali uliofanywa na wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Harvard ulibaini kwamba baadhi ya wanawake wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata watoto wa jinsia moja tu.

Katika utafiti huo, watafiti walichambua taarifa kutoka kwa zaidi ya akina mama 58,000 waliowahi kujifungua angalau mara moja.

Matokeo yao yalionyesha kuwa umri wa mama wakati wa kujifungua kwa mara ya kwanza una mchango mkubwa katika kuamua jinsia ya watoto watakaofuata.

Wanawake waliokuwa na umri zaidi ya miaka 28 walipojifungua kwa mara ya kwanza walikuwa na asilimia 43 ya uwezekano wa kupata watoto wa jinsia moja tu.

Lakini, wanawake waliokuwa na umri chini ya miaka 23 walipojifungua kwa mara ya kwanza walikuwa na asilimia 34 pekee ya uwezekano wa kupata watoto wa jinsia moja.

“Umri mkubwa wa mama unaweza kuhusishwa na uwezekano mkubwa wa kupata watoto wa jinsia moja tu, lakini mambo mengine ya kurithi, kijamii, au ya uzazi hayakuonekana kuwa na uhusiano na jinsia ya watoto,” watafiti walieleza.

Nchini Tanzania huduma ya upandikizaji mimba imekuwa ikitolewa kwa miaka mingi katika hospitali kadhaa binafsi. Mwaka 2024 huduma hiyo ilianza rasmi kutolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili, ikiwa hospitali ya kwanza ya umma kutoa huduma hiyo.

Jumla ya wenza 2000 walijitokeza kuhitaji usaidizi wa kupata watoto katika kitengo cha upandikizaji mimba (IVF) Muhimbili na kwa mujibu wa wataalamu, 120 wamebainika kuwa na vigezo vya upandikizwaji mpaka kufikia Mei mwaka 2025.

“Wamekuja mpaka watu wazima wana miaka 50 mpaka 60, lakini sasa unakuta tayari ana magonjwa, presha, kisukari unamwelekeza tu kwamba kwa afya yako nini unafaa kufanya,” amesema Mkuu wa kitengo cha IVF Muhimbili, Dk Matilda Ngarina.